TAASISI ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) itaanza kutoa huduma ya kisasa za upasuaji wa uvimbe bila kutoa viungo vya mwili baada ya wataalmu kupata mafunzo kutoka kwa madaktari bingwa wabobezi duniani.
Jumla ya wagonjwa 67 wenye tatizo la uvimbe walifika kupatiwa matibabu katika taasisi hiyo kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Mei, 2023.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo yaliyoanza jana na kumalizika kesho, Kaimu Mkurugenzi wa MOI, Dk Lemeri Mchome amesema mkutano huo umefanyika kwa mara ya kwanza nchini utaleta mbadiliko makubwa.
Dk Mchome amebainisha kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuongeza ufanisi katika kutibu wagonjwa,kuondoa usumbufu ambao wagonjwa wanapata kwenda nje ya nchi na kupunguza gharama kwa wagonjwa na taifa kutibu wagonjwa nje kwani kuna gharama nyingi.
Amefafanua kuwa pia yatafungua milango kwa nchi zinazotuzunguka kwa utalii wa matibabu kwani wataleta wagonjwa wenye uhitaji ili waweze kupata huduma.
“Leo tunamafunzo ya kimataifa na mkutano huu ni maalum na wa mara ya kwanza katika nchi yetu katika matibabu ya magonjwa ya Uvimbe unaotokea katika mfumo wa mifupa na misuli au kansa za mifupa.
Ameongeza “Tumekuwa tukitibu wagonjwa hawa tangu taasisi ilivyoanzishwa lakini matibabu yetu yamekuwa mara nyingi wagonjwa wanapokuja shida imetokea kwenye mfupa inapelekea mguu kuondolewa kabisa.
Amesema sasa wamejifunza kuwa mataifa yaliyoendela tayari wameshaanza upasuaji wa kuondoa uvimbe bila kukata kiungo hivyo wameleta kozi hiyo kujenga uwezo.
Dk Mchome amesema kutokana na mafunzo hayo wataweza kutoa huduma ambazo zinatolewa sehemu zote Duniani ambapo watabadilisha huduma ya kukata mguu kwa kubakiza viungo viendelee kuwepo.
Meneja wa Idara ya kubadilisha viungo bandi na kurekebisha ulemavu MOI, Dk Vailent Lukonda amesema wanajivunia kuwa na mafunzo hayo na yatasaidia kuwajengea uwezo kwa wataalamu wao na waliokuja ni wanafanya kazi hizo huko kwao.
“Wengi wanasema tatizo hili sio kubwa lakini lipo na wagonjwa wakija wanakuja na matatizo makubwa na inakuwa changamoto kuwatibu,”ameeleza