WAGONJWA watatu wa kiharusi (stroke) hupokelewa kila siku katika Taasisi Tiba ya Mifupa (MOI).
Daktari bingwa wa Ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu katika taasisi hiyo, Laurent Mchome amesema kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa kiharusi unasababishwa na shinikizo la juu la damu na lehemu.
“Zipo aina nyingi za kiharusi lakini wagonjwa wengi tunawapata ni wale ambao damu imevilia kwenye ubongo, tatizo hili ni kubwa sana, kwenye maabara yetu tunawafanyia uchunguzi tukiona wanahitaji upasuaji ndipo tunawafanyia upasuaji,”amesema.
Amesema miaka ya nyuma wagonjwa hao walikuwa wakipatiwa huduma saidizi na wakipata nafuu hupelekwa nje ya nchi kutibiwa lakini sasa wanatibiwa hapa nchini.
“Wagonjwa wengi wenye shinikizo la juu la damu ambao hawatumii dawa kwa kufuata mpangilio maalumu walioelekezwa na wataalam wapo kwneye hatari ya kupata ugonjwa huu
“Pia wapo wanaopata lehemu kwenye damu wapo kwenye hatari ya kupata vivimbe ambavyo hupasuka na mtu kupata kiharusi,” amesema.
Jumla ya wagonjwa 12 wenye matatizo ya kuvuja damu kwenye ubongo wamefanyiwa upasuaji katika Taasisi Tiba ya Mifupa (MOI).