MOI yatibu wagonjwa 410 Tabora

WAGONJWA 410 wamepatiwa matibabu katika kambi maalum ya matibabu ya mifupa, ubongo, mishipa ya fahamu na uti wa mgongo katika Hospitali ya Rufaa ya Nkinga iliyoko mkoani Tabora.

Huduma hizo zimetolewa na Madaktrai Bingwa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya fahamu (MOI) kwa kushirikiana na madaktari wa hospitali ya Nkinga.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kambi hiyo mkoani Tabora ,Mkurugenzi wa MOI , Dk Respisius Boniface amesema huduma hizo ni agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.

“Tuko hapa Hospitali ya Rufaa ya Nkinga kwa siku tano katika kambi maalum ya kutoa huduma za kibingwa, tunawahudumia wagonjwa kwa huduma tunazotoa, nawashukuru uongozi wa hospitali hii kwa kukubali hiki kitu kizuri ambacho serikali inataka, “ amesmea.

Dk Boniface amesema Rais Samia anataka huduma zinazopatikana Dar es Salaam zifike na mikoani, kwani sio kila mtu anaweza kufika huko hivyo wataendelea kutekeleza maagizo ya serikali  na watakuwa na mabingwa wao watakaotoa huduma na kujengeana uwezo wa kutoa huduma.

“Tunawajengea uwezo watumishi wa hapa na sisi pia wataalamu wetu wanajifunza na niseme tumeanza itakuwa mwendelezo,”amesisitiza.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali ya Nkinga, Dk Tito Chaula amesema kati ya wagonjwa 410 wagonjwa 20 walifanyiwa upasuaji na hali zao zinaendelea vizuri.

“Mwitikio ulikuwa mkubwa tumeona wagonjwa 410 hadi sasa na wengine wanatibiwa tumefanya upasuaji kwa watu 20 na zingine zinaendelea, kimsingi imekuwa huduma nzuri kwa ukanda wa magharaibi wanaotakiwa kusafiri wamepata huduma hapa watu wenye changamoto wameweza kutibiwa hapa,”ameeleza.

Amesema kupitia kambi hiyo madaktari wa ndani wamejengewa uwezo wanaweza kufanya upasuaji wa kichwa kikubwa na imeenda vizuri watoto wanaendelea vizuri.

“Huduma hii inahitajika katika huu ukanda wapo ambao hawana fedha huduma ikisogea wanapata huduma hapa tunawashukuru kwa ushirikiano mkubwa waliotuonesha, tutaendelea kutoa huduma hizi ambazo tunaweza kutoa na tutaendelea kufuatilia wagonjwa waliohudumiwa kwa ukaribu,”amesema.

Naye daktari bingwa wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu kutoka MOI , Dk Alpha Kihomela, amesema kwa mara ya kwanza wanaweza kufanya upasuaji kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi, wameweza kurekebisha mishipa ya uti wa mgongo uliokuwa umeteguka.

 

“Na mgonjwa amerudi kama alivyo zamani kabla ya kupata ajali na kijana huyu anaendelea vizuri na ingekuwa kama si kuja huku angesafirishwa kwa ajili ya matibabu, tumeokoa gharama ya kusafiri na pengine hata angeshindwa kusafiri,” amesema.

Amesema pia kuna mtoto mchanga wa siku nne ambaye alizaliwa mgongo wazi angeweza kusafirishwa, lakini amepata matibabu akiwa hapo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button