Mollel awataka wazazi kupeleka watoto shule

KILIMANJARO: MBUNGE wa Jimbo la Siha, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha miundombinu ya elimu kwa kujenga shule katika kila kijiji ili kuwapunguzia watoto adha ya kutembea mwendo mrefu kwenda shule.
Dk. Mollel amebainisha hayo wakati akiwa katika ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo iliyoletwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika Jimbo la Siha ambapo amewataka Wananchi kumuunga mkono Rais Samia kwa kuhakikisha wanapeleka watoto shule ili kupata elimu.
Amesema Rais Samia katika jimbo la Siha ameupiga mwingi hususani kwenye kuboresha miundombinu ya elimu na madarasa mengi yamejengwa katika shule zilizokuwa zimechakaa na kuleta taswira mpya katika jimbo hilo.
“Mpaka sasa tumebaki na vijiji vichache sana ambavyo havijapata shule ila naimani kubwa kwa dhamira ya kiongozi wetu Dk. Samia kabla ya 2025 atakuwa ameweka mambo safi”, ameeleza Dk. Mollel
Aidha ameeleza kuwa serikali imara ya Samia inaendelea kuhakikisha inaleta maendeleo kwa wananchi wake kwa kuhakikisha inaboresha miundombinu ya barabara, upatikanaji wa maji pamoja na umeme ili kuwatia moyo wananchi kuendelea kufanya maendeleo katika taifa lao.