Mongella asifu uwezo wa Samia

MWANASIASA mkongwe, Balozi Getrude Mongella ametaja mambo ambayo wanawake wanapaswa kuyazingatia wakubalike kiuongozi, wawe imara kama Rais Samia Suluhu Hassan alivyomudu kuongoza nchi.

Mongella amesema wanawake wengi wanafunika vipaji vyao kwa kuzoea kudidimizwa na mila, desturi kiasi cha kushindwa kujionesha, kuonea aibu uongozi wakidhani ni sifa.

Alisema hayo nyumbani kwake Makongo Juu, Dar es Salaam kwenye mahojiano maalumu na waandishi wa habari wa kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN).

“Wengi (wanawake) tunaficha vipaji vyetu, hata kama tunajua kuongoza hivi, tunakuwa kama aibu ni sifa, kutojionesha ni sifa, kumbe uongozi unahitaji ujitoe, ujioneshe.

“Ndio maana ukiangalia katika orodha ya niliyofanya nilijitutumua. Usifiche vipaji. Kututumuka kumo, kujiamini kumo,” alisema Balozi Mongella na kuongeza:

“Lazima ufanye vitu vinavyokufanya uwe ni yule (jamii ikukumbuke), hata ukitamkwa, hakuna anayezimia. Na kwa sisi wanawake ni ngumu zaidi kwa sababu, ukitamkwa, na huna vigezo, tunatungiwa mambo mengi kweli…si yule mchepuko wa fulani. Kwa hiyo, ili uweze kusimama imara kama alivyosimama Mama Samia, lazima historia yako ina vitu…si yule, si alifanya hiki,”

Alisema Rais Samia ameonyesha kipaji cha kuongoza, uwezo wa uongozi na aliaonza kwa kujitolea,akaonekana na kuanza kupewa majukumu.

Mongella alikuwa Katibu Mkuu wa Kongamano Kuu la Umoja wa Mataifa la Wanawake Beijing, China mwaka wa 1995 na amesema ‘ukimwangalia Samia, mimi nimemfahamu kama binti tu, siwezi kusema ni wa rika langu na hata kikazi sipo katika rika lake. Na hata tulivyoenda Beijing, yeye alikuwa amejitolea, alitusaidia sana kundi la akina mama wazee waliotoka Zanzibar”.

Alisema Rais uwezo wa Samia ulimwezesha kupewa jukumu la kuongoza Bunge la Katiba na baadaye akafikiriwa kuwa Makamu wa Rais kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania.

“Huyu mtu si aina ya wale wa kusema mimi hiyo kazi siwezi. Anajiamini, anajituma kwa sababu kazi ya Bunge la Katiba ilikuwa na shughuli nyingi za kujituma. Lazima ujitume, lazima ujifunze nina uhakika alikuwa makini kupitia katiba za nchi nyingine na ya kwetu ili kupata kuongoza mazungumzo yaliyofanywa.”

Alisema kama ingetokea akapendekezwa mwanamke ambaye hana chochote alichowahi kufanya, awe Makamu wa Rais, ni dhahiri watu ‘wangezimia’.  “Lakini alipopendekezwa hakuna aliyezimia, lazima ufike iwe ni yule…Lazima ufanye vitu vinavyokufanya uwe ni yule.”

Amsifu Samia

Mongella alisema, “kilichomtokea, wote tunataka uongozi lakini si kwa namna alivyopata uongozi. Unaamka asubuhi wanakuambia kiongozi wako amefariki… Watu tulivyosikia Magufuli (Rais John) amefariki, mimi sikulala. Nilikuwa nimekaa kwenye kiti, kumekucha nimekaa hivyo hivyo sijui kwa nini.”

Alisema ni tukio ambalo Watanzania hawakuwahi kufiwa na kiongozi aliye madarakani. Alisema Rais Samia alikuwa na wakati mgumu kwa kuwa alipewa uongozi katika mazingira ambayo watu hawakuamini kilichotokea.

“Mazingira ambayo leo tunasema nani, nani? Kwa sababu wengine hata Katiba walikuwa hawaisomi, ya kusema anapofariki kiongozi aliyeko madarakani nini kinafanyika? Wengi walikuwa hawajui; hata viongozi.”

Mongella alisema: “Kwa hiyo wengine walianza na kutamani (urais), mpaka ukiambiwa hii kikatiba ni Makamu wa Rais kwa maana hiyo ni Samia Suluhu Hassan full stop. Lakini wangeiacha bila kuieleza kikatiba…nadhani mtupongeze, Katiba yetu tuliiandika vizuri. Bila kuieleza katika katiba, angeweza kutupiliwa mbali.”

Alisema Samia alishika uongozi katika mazingira magumu yaliyojaa sintofahamu, kukiwapo waliohoji kama ataweza, wengine wakitaka kumfahamu ni nani.

Alisema hali hiyo ni wazi ilimfanya mbali na kuhangaika kutafuta mbinu, uzoefu na maarifa ya kuongoza nchi, pia alipambana na dhana hizo ambazo Mongella ameziita ‘makandokando’.

Shujaa, anajiamini

Hata hivyo, Mongella alisema Rais Samia amepambana kikamilifu na kudhihirishia umma tangu siku ya kwanza. “Kiongozi ni ushujaa, lazima ujiamini, kajiamini tangu siku ya kwanza aliposema, mimi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika umbile la mwanamke. Mimi hapo nilipiga vigelegele, alitoa kauli nzito.”

Aliongeza, “kwa sababu angeanza, mimi jamani ni mwanamke naomba mnisaidie…mie ningesikitika sana.”

Balozi Mongella alisema anamuona Samia anatutumuka (kuthubutu) kama ambavyo yeye alipenda kututumuka na kushika nafasi mbalimbali kitaifa na kimataifa.

Alitoa mfano kuhusu ajenda ya Samia ya kurudisha watoto wanaopata mimba shuleni na kusema, “si wote tuliielewa. Kuna mambo mengi ambayo yanatushinda kuelewa mpaka tunapoona, …tunakuwa kama Thomaso aliyegusa katika vidonda vya Yesu ndipo akasema kumbe ni wewe Bwana.”

Amefanya mazito

Alilinganisha simulizi hiyo ya kwenye Biblia akisema, watu wengi wamethibitisha urais wa Samia kwa kuona mambo mazito aliyofanya katika kipindi kifupi.

“Tumuombee Mungu ampe afya njema na Kazi Iendelee kama anavyosema mwenyewe. Wanawake mnaweza kuingia katika mazingira yoyote, tuache woga. Katika mazingira yoyote yatakayokukuta ni lazima tuwe imara kuchukua nafasi za uongozi hamna kurudi nyuma. Iwe imetokea kama ya Samia, ama iwe imetokea umechaguliwa,” alisema.

Alitoa mfano wake alivyoteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo, Boutros Boutros-Ghali, akisema licha ya kuhofu kutokana na ukubwa wa nafasi, lakini aliimudu.

Alisema miaka iliyopita wanawake wengi vipaji vyao vilikufa kwa sababu ya woga huku jamii ikichangia.

Alisema miongoni mwa wakwamishaji ni ndugu, marafiki ambao wakati mwingine hufanya hivyo kwa sababu ya wivu. Alisisitiza mwanamke kuwa jasiri kwa kutokubali kurudishwa nyuma.

Chagua wanaofaa

Akizungumzia kuchagua viongozi wanaofaa, Mongella aliwataka wananchi kutoacha mwanya kwa watu wasiofaa kushika uongozi kwa kutokwenda kupiga kura au kwa wanaofaa kutogombea.

“Ukitaka, tungoje mwaka kesho, unakuta wasiofaa ndio wamehamasika. Wewe unayefaa unasema shauri yao, na hasa sisi wanawake tunafanya hivyo,” alisema Mongella na kueleza kitendo hicho kuwa si uzalendo.

Wanawake wapigania uhuru

Aidha, Mongella ameshauri utengenezwe utaratibu wa kuwakumbuka wanawake wapigania uhuru nchini na Afrika kwa kuwatuza kutokana na ushiriki wao katika ukombozi wa bara.

Kwa upande wa Tanzania, alimtaja Bibi Titi Mohamed na Bi Mwanaidi Mohamed wa Zanzibar kuwa wanastahili kupewa tuzo. Aliwataja wanawake wengine wa nchini Msumbiji, Angola, Zimbabwe na Afrika Kusini wanaostahili kutuzwa kwa mchango wao.

Ukombozi vijana

Akizungumzia vijana, Mongella ameitaka jamii kutazama upya mawazo juu ya kundi hili kwa kile alichosema wanashindwa kwa sababu ya kuwa na mapingamizi mengi.

“Wazee tunawadharau, hatuwasaidii…nawaruhusu vijana waangalie CV yangu (wasifu) waseme hivi huyu bibi aliwezaje…sikuwa bibi mimi, nilikuwa Getrude,” alisema.

Alisema wakati anaongoza Kongamano Kuu la Umoja wa Mataifa la Wanawake Beijing la mwaka 1995, ndio alitoka kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa kutimiza miaka 50.

“Sasa mimi kwangu sijaona kuwa ujana ni kizuizi cha kufanya mambo nitakayo. Katika ujana niliona zaidi fursa ya kwamba ni wakati wa mimi nichakarike, nifanye na nipate vitu vingi kwa wakati mmoja,” alisema Mongella.

Balozi Mongella alisema kutokana na kuwa na nguvu za ujana, aliingia katika Bunge la Afrika Mashariki akiwa ananyonyesha mtoto wake wa tatu mwaka 1975, wakati huo akiwa na miaka 30 na aliweza kutekeleza majukumu yake kama kawaida.

Alisema wakati huo ilikuwa ni kitu cha ajabu kuacha mtoto ndani na kwenda bungeni, lakini aliweza kufanya na kukamilisha majukumu yake kwa kuwa umri wake ulikuwa bado mdogo na ulimwezesha kufanikisha malengo yake.

Mongella alisema pamoja na kwamba vijana wana nafasi kubwa ya kutengeneza maisha yao mapema, bado wanakabiliwa na ubaguzi kutoka katika jamii na kwamba akipata nafasi atawaita vijana na kuwaambia hali halisi ilivyo sasa.

Balozi Getrude aliwataka wazazi na walezi kuwasaidia vijana kimawazo wasijione kuwa mahali walipo ndio mwisho wa maisha badala yake waione fursa iliyo mbele yao na namna wanaweza kuifuata na kuikamata fursa hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button