Mongella: Vyuo viimarishwe elimu yenye weledi

MKUU wa Mkoa wa Arusha ,John Mongella ameiomba Wizara ya Maendeleo ya Jamii kuviimarisha vyuo vya maendeleo ya jamii ili viweze kutoa elimu kwa utaalam na weledi katika ngazi ya cheti na diploma.

Mongella ametoa ombi hilo wakati akizindua kumbi tatu za mihadhara, darasa la kompyuta na kuweka jiwe la msingi katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii wilayani Monduli ambapo amesema kwa kufanya hivyo wataweza kuziinua kada zilizopo chini kabisa ambazo ndizo zinaonekane kuchangia uchimi wa nchi kwa kiasi kikubwa.

“Kada ambazo zinasukuma sana uchumi na kuchangia maendeleo ni kada hizi ambazo ziko chini kwasababu vijana walio wengi ndiyo wanaohitaji cheti na diploma kwasababu ndiyo ambao tunawahitaji katika utendaji.”

“Vyuo vyetu hivi vya kada mbalimbali kazi yao kubwa ni kutengeneza jamii yenye uwezo,na sasa hivi nyenzo kubwa kupita zote ni elimu,utaalam,uweledi pamoja na kutengeneza uelewa wa mambo.”

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya wa Monduli ,Joshua Nassari amesema kuwa katika vyuo vya maendeleo ya jamii ndivyo vinavyotoa taaluma za namna bora ya kushughulika na changamoto za kimaadili ambazo zinaikumba dunia ikiwemo mmomonyoko wa maadili.

“Niendelee kutoa msisitizo kwa mkuu wa chuo cha maendeleo ya jamii na wakufunzi kwamba wakati wanaendelea kutoa taaluma hii kwa wanafunzi wao ni vyema wakaangalia namna bora ambayo taaluma hii inafika kwa wanajamii”

Awali akitoa taarifa za utekelezaji wa mradi huo Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Monduli ,Boniface Daniel amesema mradi huo umegharimu kiasi cha zaidi ya fedh sh, milioni 46 ambapo kazi hiyo imekamilika kwa asilimia 100 na kuongeza kuwa chuo hicho pia kinaendelea na ujenzi wa ukumbi mpya wa mihadhara wenye uwezo wa kubeba wanafunzi 450 kwa gharama ya sh,milioni 53 na mradi umefikia asilimia 90.

Mradi huo utaongeza udahili kwa wanafunzi wanaojiunga na chuo kutoka 711 waliopo sasa hadi kufikia wanafunzi 1,150 kwa mwaka wa masomo 2023/24 na kusisitiza kuwa chuo hicho kimekuwa kikishirikiana na jamii katika upatikanaji wa fursa za ajira ikiwemo kazi ya ufundi ujenzi ,ufundi umeme ambapo hadi sasa wananchi 257 wamejipatia ajira katika mradi huo wa ukarabati na upanuzi wa darasa pamoja na ujenzi wa ukumbi wa mihadhara.

Habari Zifananazo

Back to top button