CHAMA cha Mapinduzi (CCM, Wilaya ya Morogoro kimemuomba Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kufikisha kilio cha wananchi kwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuhusu mawaziri watano wanaodaiwa kumiliki idadi kubwa ya mifugo, ili waiondoe kunusuru uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji vinavyosaidia mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
Mwenyekiti CCM wa Wilaya hiyo , Gerold Mlenge alitoa ombi hiyo kwa Waziri Aweso Januari 4, 2023 kwa niaba ya wananchi alipofanya ziara ya kutembelea, kukagua na kuzindua ujenzi wa miundombinu ya mradi wa maji katika Kata ya Lundi, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
Mlenge amesema kwa asili yake halmashauri ya Morogoro haina eneo la ufagaji bali ni ya kilimo cha mazao mbalimbali, lakini kwa sasa wafugaji wengi wavamizi maeneo ya ardhi inayotumika kwa kilimo na mifugo hiyo kukaharibu mazingira na vyanzo vya maji ikiwa pamoja na kusababisha migogoro baina ya wafugaji na wakulima.
“ Uwepo wa wingi wa mifugo umedhihirisha kuharibu vyanzo vya maji na kusababisha kuwepo kwa migogoro baina ya wakulima na wafugaji inayotokana na kugombea matumizi ya ardhi na kwa ujumla jambo hili linaweza kupatiwa ufumbuzi,” amesema Mlenge.
Alimuomba Waziri Aweso kuyachukua majina ya mawaziri hao kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, ambaye alifikishiwa taarifa na majina hayo ambaye aliahidi kuyafanyia kazi.
“Isifike mahali nikaita press ( mkutano na waandishi wa habari ) nikawataja kwa majina, naomba muende mkanong’onezane watoe mifugo yao huku Morogoro vijijini hatuna asili ya mifugo, sisi kazi yetu ni kulima, hatutaki migogoro, hatutaki migogoro ya wakulima na wafugaji,” anasema Mlenge.
Naye Chifu Kingalu wa Waluguru Mwanabanzi wa 15, amesema Mkoa wa Morogoro ni mkoa wa kimkakati katika chakula, miundombinu barabara na upatikanaji wa maji kwa ajili ya uzalishaji wa umeme.
Kutokana na hali hiyo amekerwa na tabia za baadhi ya viongozi wa serikali waliopewa dhamana wakiwemo mawaziri kufanya shughuli za ufugaji katika sehemu za vyanzo vya maji.
“ Ng’ombe zilizopo ukanda wa Morogoro Kusini sio za wananchi wa maeneo hayo, bali ni za baadhi ya mawaziri wenzako, viongozi wa serikali na wakuu wa idara ambao wanajulikana …kwa nini zisiondoshwe hizo ng’ombe, “ alisema Chifu Kingalu.
Kwa upande wake Waziri Aweso akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lundi amesema , changamoto ya uhaba ama ukosefu wa maji ni kutokana na kuharibiwa kwa vyanzo vyake mara kwa mara kunakosabishwa na suala la mifugo.
Waziri Aweso amewaahidi wananchi hao kuliwasilisha bila kukosa kwa Rais Dk Samia lalamiko lao juu ya mawaziri watano, wanaodaiwa kumiliki mifugo mingi wilayani humo.
“Mmenipa ombi maalum na viongozi wa chama wa wilaya hii juu ya changamoto ya mifugo, nikiri kulipokea na nitalipeleka kama lilivyo kama mlivyotaka, mimi ni muathirika pia,” amesema Aweso