Morogoro kuwekwa mazingira wezeshi uwekezaji

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima  amewataka wadau wa sekta ya biashara na uchumi kushikamana katika kuweka mazingira wezeshi ambayo yatawavutia wawekezaji kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ili kuzalisha ajira na kuinua pato la kuchumi la mkoa  na taifa.

Malima alisema hayo  juzi Juni 15, 2023  hotuba  yake ya ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Morogoro .

Alisema kuwepo mazingira mazuri ya biashara yanavutia wawekezaji kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali na  kufanya ukuaji wa pato la mkoa kutokana na  kodi mbalimbali zinazokusanywa kwa wafanya biashara hao.

“Tuendane na malengo yetu ya kutengeneza mazingira wezeshi, mazuri zaidi ambayo ndiyo msingi wa maelekezo ya Rais wetu Dk  Samia Suluhu Hassan” alisema Malima.

Katika kufikia malengo hayo, Malima  aliwataka  wakuu wa taasisi za umma na binafsi kufanya kazi kwa umoja kwa kuthamini mchango unaotolewa na kila mmoja ili kufanikisha maendeleo ya mkoa huo.

Mkuu wa mkoa pia  alimshukuru na kumpongeza Rais Dk Samia kwa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kuwekeza kwenye miradi mikubwa  ikiwa na kuondoa changamoto za uwekezaji.

Malima  alimpongeza Rais kwa kuchukua hatua za kuhakikisha ya kwamba wafanyabiashara wanakuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi.

Mkurugenzi wa Idara ya Masoko wa Kampuni ya Sukari Kilombero , Fimbo Butallah alisema kiwanda kinafanya upanuzi ili kuongeza uzalishaji wa sukari na kutoa fursa za ajira kwa wananchi wa mkoa huo.

Alisema licha ya kutoa ajira, kiwanda kinapata malighafi ya miwa kutoka kwa wakulima zaidi ya  8,000 ambao wanazalisha  wastani wa tani 600,000 za miwa kwa mwaka.

Butallah  alisema kupitia upanuzi wa kiwanda hicho , mahitaji ya miwa yataongezena  na hivyo watahitaji wakulima zaidi 1,400  kulima miwa ili kufikisha tani  milioni moja na nusu za miwa kwa mwaka  kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kiwanda hicho.

” Kwetu sisi Kiwanda Cha Sukari Kilombero tutaendelea kudhamini mikutano ya biashara  kama hii ili kufungua fursa za kiuchumi za mkoa  wa Morogoro na Taifa”alisema Butallah

Habari Zifananazo

Back to top button