Moto wateketeza bweni Bukoba
KAGERA: Moto ambao chanzo chake hakijajulikana umeteketeza bweni moja katika shule ya sekondari ya wasichana Omumwani Iliyoko kata ya Nshambya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera na kupelekea mali za wanafunzi na thamani zilizoko katika chumba hicho kuungua.
Bweni hilo limelipuka moto majira ya saa 2.30 usiku na kusogeza wananchi waliosaidiana na jeshi la Zima moto na Uokoaji kuzima moto huo haraka ili usilete madhara zaidi kwa shule na wanafunzi kwa ujumla.
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Erasto Siima akizungumza na wananchi na wanafunzi kwa ujumla amesema kuwa hakuna madhara ya wanafunzi kuungua isipokuwa wanafunzi wamepata mshutuko na wanaendelea na uchunguzi katika kituo cha afya cha Zamuzamu.
Kamanda wa jeshi la Zimamoto na Uokoaji Zabron Muhumuha amesema kuwa uchunguzi wa chanzo cha moto huo unaendelea na taarifa kuhusu chanzo cha moto na ukubwa wa tatizo zitatolewa.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Kagera Blasius Chatanda ametoa wito kwa wananfunzi kutoa ushirikiano pindi uchunguzi utakapokuwa unaendelea na kubainisha kuwa kama kutakuwa na uhalifu umetekelezwa hatua za kisheria zitachukuliwa.