Motsepe: Bao la Aziz Ki lilikuwa halali

ZANZIBAR; RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe amesema bao alilofunga Aziz Ki wa Yanga katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi lilikuwa halali.

Motsepe amesema hayo leo baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume mjini Zanzibar, ambapo usiku anatarajiwa kufunga fainali za African Schools Football Championship Uwanja wa Amaan Complex usiku.

“Nilipokutana na Rais Wallace (Karia) baada ya mechi ya Mamelodi dhidi ya Yanga nilimwambia nafikiri lile lilikuwa ni goli halali, lakini siwezi kuingilia maamuzi ya waamuzi na kamishna,” amesema Motsepe na kuwafanya watu kuangua kicheko.

“Ubora wa soka Tanzania na Zanzibar ni mkubwa kwa sasa na wavulana na wasichana wa timu yao wanacheza fainali, jambo linalodhihirishia ulimwengu ubora wa Afrika na kuwapa kujiamini kuwa timu za Afrika zinaweza kushinda Kombe la Dunia, ” amesema.

Amesema kuwa soka la Tanzania linakua jambo linalodhihisha ubora wa Afrika na kuwafanya viongozi kujiamini.

Amesema anajivunia uongozi wa soka wa Tanzania na ushirikiano wao na serikali, ambao umefanya kuandaa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.

Katika mashindano hayo timu ya wavulana ya Tanzania itacheza fainali dhidi ya Guinea baada ya kuifunga Benin 2-0 katika mchezo wa Nusu Fainali na Guinea iliifunga Senegal kwa penalti4-3 baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu.

Timu ya wasichana ya Tanzania itacheza mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu dhidi ya Uganda, baada ya Tanzania kufungwa na Afrika Kusini 1-0 na Uganda ilifungwa na Morocco 1-0. Mashindano hayo yalianza kutimua vumbi Mei 21mwaka huu.

Habari Zifananazo

Back to top button