MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ameliagiza Jeshi la Kujenga Taifa kutowalea wanaodaiwa takribani Sh bilioni 19 baada ya kupewa huduma ya ulinzi na Kampuni ya SumaJKT Guard.
Pia alimuagiza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa kukaa na Waziri wa Fedha na Mipango, mawaziri wa kisekta na wakuu wa taasisi zinazodaiwa kuangalia namna ya kuhakikisha deni hilo linalipwa.
Dk Mpango alitoa agizo hilo wakati wa kutembele mabanda ikiwa ni maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa JKT Julai 10, 1963 baada ya kupewa maelezo na Mkuu wa SumaJKT Guard, Kanali Joseph Masanja.
Masanja alisema pamoja na kuwa na mikataba na washitiri wao, baadhi ya taasisi hususani za umma wamekuwa wagumu kulipa hatua ambayo inaifanya mpaka sasa kudai zaidi ya Sh bilioni 19.
Dk Mpango alimuagiza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Bashungwa kukaa pamoja na mawaziri wenzake na wakuu wa idara kuangalia namna ya kulimaliza deni hilo ambalo alisema limekuwa likichangia kuzorotesha utoaji wa huduma.
Alimtaka pia Bashungwa kukutana na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Mchemba kuangalia namna ya kulimaliza deni hilo.
Baadhi ya taasisi ambazo zinataiwa na SumaJKT Guard ni Kampuni ya madini ya Tulawako, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Wakala ya Ufundi na Umeme (TAMESA)-Pwani, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Dar es Salaam(DAWASA) na Hospitali ya Taifa ya Mloganzila.