MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ameagiza wananchi waliojenga katika vyanzo vya maji vya milima wapatiwe maeneo mengine ya kujenga na waondoke mara moja ili kutunza uendelevu wa vyan
zo vya maji. Ametoa maagizo hayo jana katika ufunguzi wa Mkutano wa Nane wa Mwaka wa Bodi za Maji za Mabonde unaofanyika jijini hapa. Mkutano huo umebeba kaulimbiu ya ‘Utunzaji ende
levu wa vyanzo vya maji kwa ustawi wa jamii na ukuaji wa uchumi.’ Dk Mpango alisema ili kusimamia rasilimali za maji ni lazima wananchi, viongozi wa vyama na serikali pamoja na wataalamu wa sekta zote kushirikiana kusimamia kikamilifu maeneo yote ya vyanzo vya maji yaliyoainishwa na yawekewe mipaka.
“Kwenye hili nataka nisisitize kwa mara nyingine tena wananchi waliojenga katika vyanzo vya maji vya milima kama ile Uluguru katika Mkoa wa Morogoro na mikoa mingine, hawa wapatiwe maeneo mengine ya kujenga na waondoke katika vyanzo hivyo haraka iwezekanavyo,” alisema Dk Mpango.
Aidha, ameziagiza Wizara za Fedha na Mipango na ile ya Nishati kukaa na kujadili mpango wa kupunguza gharama ya gesi nchini ili wananchi wengi wamudu gharama hizo na kuondokana na matumizi ya mkaa ambayo kwa kiasi kikubwa yanaathiri upatikanaji wa maji kutokana na ukataji wa miti.
Dk Mpango ameiagiza Wizara ya Kilimo kwenda kufanya utafiti wa kina katika mabonde ya mito mikuu ya kimkakati kama Ruaha na kubaini wamiliki wa mifereji ya maji ya umwagiliaji na kujua kiasi cha maji yanayochepushwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema wizara itaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wa serikali katika kutunza vyanzo vya maji.
Aweso amebainisha kuwa maji yanayopatikana chini na juu ya ardhi ni mita za ujazo bilioni 126, bilioni 105 zikipatikana juu ya ardhi na bilioni 121 chini ya ardhi.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete alisema wizara itaendelea na utekelezaji wa maagizo ya Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu katika kuhamisha wananchi waliovamia maeneo ya mabonde ya vyanzo vya maji na wale ambao mipaka imewafuata wameandaliwa utaratibu wa fidia.
Comments are closed.