Mpango akerwa ukatili kwa watoto/ukahaba

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ameviagiza vyombo vya dola viongeze nguvu kupambana na ukatili dhidi ya watoto wa kike na wa kiume.

Aidha, Dk Mpango amekemea vitendo vya ukahaba, mimba za utotoni na dawa za kulevya huku akitaja sababu matukio hayo kuwa ni malezi dhaifu, utandawazi holela na umasikini katika kaya.

Alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la Maadili la Viongozi wa Dini wa Kamati za Amani na Jumuiya ya Maridhiano Tanzania.

Dk Mpango alisema taifa limeendelea kushuhudia vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na kuripotiwa mara kwa mara katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Dk Mpango alisema takwimu za Jeshi la Polisi za mwaka 2021, zinaonesha kulikuwa na matukio 5,899 ya ubakaji, mimba za utotoni 1,677 na ulawiti matukio 1,114.

“Najiuliza hofu ya Mungu imepotelea wapi na kwa maoni yangu haya yote yametokana na mmomonyoko wa maadili hivyo lazima kama jamii itambue haki za msingi za mtoto ikiwemo kuishi, kulindwa, kuendelezwa na kutobaguliwa,” alisema Makamu wa Rais.

Alisema watoto ni hazina kwa taifa hivyo kuwe na mifumo imara ya ulinzi katika ngazi ya familia, mtaa, shuleni na vyuoni ili kulinda haki na ustawi wa watoto hao.

Alisema ni muhimu kukemea vitendo hivyo bila aibu wala woga hivyo wazazi wachukue hatua na wasilindane badala yake wawafichue wahusika.

Aidha, alisema ukahaba umezidi kuenea na haukubaliki katika mila, desturi na dini zote na kwamba wazazi kutokuwajibika ipasavyo kumechangia watoto na vijana kujihusisha na vitendo hivyo.

Pia alisema ukatili dhidi ya wanawake ni kinyume cha maagizo ya Mwenyezi Mungu na ni kikwazo kwa maendeleo jumuishi na endelevu. Alisema matukio ya unyanyasaji dhidi ya wanawake yaliyoripotiwa kwa mwaka 2021 ni 20,897 na mwaka 2020 yalikuwa 28,126 na kwamba anaamini zipo kesi nyingi ambazo hazikufika kwenye vyombo vya dola.

“Mkiwa viongozi wa dini sauti zenu zinaheshimiwa sana hivyo mshirikiane na serikali katika kupaza sauti kukataza mila na desturi katili, zinazodhalilisha na kumnyima mwanamke haki zake,” alisema Dk Mpango.

Aliongezal: “Lakini hivi karibuni tumesikia wanaume ambao wanafanyiwa vitendo vya ukatili na wake zao hadi kuanzisha chama cha kuwaunganisha kupinga ukatili na dhuluma wanazofanyiwa hivyo hatupaswi kufumbia macho ukatili huu.” Kuhusu mimba za utotoni na watoto wa mitaani, alisema bado lipo na sababu ni baadhi ya wazazi kuacha jukumu lao la kulea watoto, kuvurugika kwa ndoa hivyo watoto kulelewa katika mazingira yasiyoridhisha.

Alisema hali hiyo imechangia watoto kuingia katika makundi hatarishi kwa kuacha shule, kujihusisha na wizi, ujambazi, ulevi, vitendo vya ngono hata juu ya makaburi kitu ambacho ni laana.

Alisema vijana wengi wamekufa kwa sababu ya matumizi ya dawa za kulevya, na jambo hilo linaathiri afya za vijana, jamii na uchumi kwa ujumla na kuhatarisha ulinzi na usalama wa nchi.

“Vijana wengi ukiwauliza kuhusu tabia hizi watakwambia kuwa wamefundishwa na ndugu, jamaa, marafiki, wageni na wafanyakazi wa majumbani, husababisha madhara makubwa kiuchumi na kijamii. Vijana wakifundishwa mila na desturi sahihi pamoja na kushika mafundisho ya dini watakuwa na hofu ya Mungu hivyo maovu mengi yatapungua,” alisema Dk Mpango.

Habari Zifananazo

Back to top button