Mpango: Andikeni wosia kulinda wajane, yatima

Dk Mpango.

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ametoa mwito kwa jamii ione umuhimu wa kuacha wosia ili wajane na yatima wasidhulumiwe mali.

Dk Mpango alisema hayo katika Kiwanja cha Ndege cha Dodoma wakati yeye na mkewe, Mbonimpaye Mpango walipoungana na watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais kuaga na kuusindikiza mwili wa aliyekuwa mtumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Emmanuel Majanja.

Majanja aliaga dunia kwa ajali ya gari Aprili 28, mwaka huu katika eneo la Mbande mkoani Dodoma.

Advertisement

Mwili huo ulisafirishwa kupelekwa Ukerewe mkoani Mwanza kwa ajili ya mazishi.

“Katika misiba mingi tunamkosea Mungu kwa kutojali sana wajane, kwa kutowajali yatima.

Hapo tunamkosea Mungu…inapowezekana ni vema sana kuacha hata maandishi mapema kwamba mimi siku zangu zikifika basi vitu hivi ambavyo nimechuma pamoja na mwenzangu mgawanyo wake upo hivi, hivi, hivi,” alisema Dk Mpango na kuongeza:

“Na mkavipeleka kwa wanasheria au benki vikahifadhiwa. Sijui binadamu tunakuwaje, tunakuwa na hulka za kunyang’anya hata mali za watoto yatima, sio kitu kizuri hata kidogo.

Akina mama wajane ndio waliotuzaa sisi wanaume, walizaa kila mmoja wetu. Sio jambo zuri kuwanyanyasa wajane, tunakosa baraka.”

Alisema Majanja alifanya kazi yake vema na kwa bidii kubwa na akasema ni vema kuendelea kujifunza kuishi vema kwa kutengeneza marafiki wengi zaidi ya maadui na kutambua siku za kuishi duniani si nyingi.

Dk Mpango alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa faraja aliyotoa kwa Ofisi ya Makamu wa Rais tangu usiku ilipotokea ajali na ametoa ndege kwa ajili ya kusafirisha mwili wa Majanja.

“Ni mama wa mfano sio kwa cheo chake, ana utu, nadhani ni mfano kwa sisi wengine viongozi, kujishusha na kulia na wanaolia,” alisema.