Mpango ataka mawakili wanaosumbua wawajibishwe

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ametoa wito kwa Chama Cha Mawakili Tanganyika (TLS) na Kamati ya Mawakili kuchukua hatua kali za kinidhamu na kisheria dhidi ya mawakili wote wanaoharibu heshima ya taaluma ya sheria kwa kukosa uadilifu na maadili mema.
 
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa TLS uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) leo Mei 11, 2023, Dk Mpango alikemea tabia ya baadhi ya mawakili kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa na kuharibu kesi wanazoletewa.
 
“Kumekuwa na tuhuma za baadhi ya mawakili kujihusisha na vitendo vya rushwa na udanganyifu kwa maslahi yao binafsi ikiwemo kuwasaliti wateja kwa kupokea rushwa kutoka upande wa pili,” Alisema Dk Mpango.
 
Aidha, aliwaambia TLS kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria kutoa elimu kwa umma kuhusu suala la mihuri ya kielektroniki ili kuondokana na suala la vishoka na mawakili wanaotumia mihuri isiyo halali kufanya kazi za uwakili.
 
Kwa upande mwingine aliziambia sekta na taasisi za sheria ziendelee kuchambua, kubaini na kutoa mapendekezo ya sheria zinazotakiwa kufanyiwa marekebisho au kuandikwa upya.
 
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro ametoa wito kwa wanachama wa TLS kushiriki kikamilifu katika mchakato wa katiba mpya pamoja na mchakato wa mabadiliko ya sheria zinazohusiana na siasa, uchaguzi na demokrasia.
 
“Wanachama hao ni wadau muhimu katika kuhakikisha inapatikana katiba mpya itakayoweza kusaidia taifa miaka mingi ijayo,” alisema Dk Ndumbaro

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x