Mpango ataka siasa za kistaarabu

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amewataka Watanzania watumie fursa ya mikutano ya kisiasa kufanya siasa za kistaarabu ili kuendeleza amani na utulivu uliopo nchini.

Alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lilondo kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma wakati alipowasili kuanza ziara ya kikazi katika mkoa huo juzi.

Dk Mpango alisema sio jambo jema kutumia lugha zisizo na staha wakati wa kufanya shughuli za siasa kwani hupelekea uvunjifu wa amani na utulivu.

Advertisement

Katika hatua nyingine, Dk Mpango alisema mwaka huu wa fedha serikali itajenga barabara ya Litukila – Songea kilometa 98 ili kukabiliana na changamoto za miundombinu mkoani humo.

Aliagiza pia Wizara ya Maji kupeleka Sh milioni 150 katika Kijiji cha Lilondo zitakazowezesha usambazaji wa miundombinu ya maji ili kutoa huduma kwa wananchi wa eneo hilo.

Akiwa katika Kijiji cha Mlilayoyo kilichopo Namtumbo mkoani humo, Dk Mpango alikemea uingizwaji kwa wingi mifugo hususani ng’ombe hali inayochochea uharibifu wa mazingira.

Aliuagiza uongozi wa Mkoa wa Ruvuma kufanya tathmini ya mifugo iliyopo na uwezo wa mkoa huo katika kupokea ng’ombe hizo.

Dk Mpango aliwataka pia wananchi wa mkoa huo kuwa makini wakati wa kuuza mazao hususani ya chakula ili kuhakikisha wanabaki na akiba ya kutosha.

2 comments

Comments are closed.