Mpango ataka tathmini bei ya kuchimba visima

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ameagiza ifanyike tathmini ya bei zinazotumika na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuchimba visima vya wananchi ili zisiwe za juu zaidi ya bei za kampuni binafsi.

Dk Mpango alitoa agizo hilo wakati akikagua magari na mitambo ya uchimbaji visima na mabwawa yaliyokabidhiwa kwa Ruwasa.

Alikagua magari hayo Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya uzinduzi wa taarifa ya utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa mwaka 2021/2022, aliagiza pia mitambo ya uchimbaji visima iliyonunuliwa na serikali itumike kwa matumizi yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na huduma kwa wananchi kwa gharama nafuu.

Ameagiza mamlaka za maji zitoe kipaumbele kupeleka maji safi maeneo muhimu ya kutolea huduma za kijamii zikiwemo hospitali, nyumba za ibada, vituo vya afya na shule.

Katika hatua nyingine Dk Mpango ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) iongeze nguvu kufanya ukaguzi wa ankara za maji zinazotolewa kwa wateja wa mamlaka za maji nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button