Mpango awaonya UVCCM kutotumika kisiasa

KIGOMA: MAKAMU wa Rais Dk Philip Mpango ameitaka Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kuepuka kutumika kutengeneza makundi yanayochangia kutengeneza vurugu katika chama na jumuiya zake.

Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo mjini Kigoma katika kongamano la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyofanya kwa kipindi cha miaka mitatu madarakani ikiwa sehemu ya ratiba kuelekea kikao cha baraza kuu la UVCCM litakalofanyika  jumanne wiki hii mkoani Kigoma.

Dk Mpango amesema kuwa ni lazima viongozi wa UVCCM na wanachama wa jumuiya hiyo kuepuka kutumika kisiasa na kujiingiza kwenye mambo ambayo yatasababisha vurugu na  kuharibu amani yetu.

Advertisement

Makamu huyo wa Rais amesema kuwa ustawi wa chama unachangiwa na jumuiya zake ambazo ni imara, hivyo ametoa  wito kwa UVCCM kuendelea  kuungana na kushikamiana ili kuijenga jumuiya iliyo bora na yenye nguvu.

Katika kongamano hilo Makamu wa Rais kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan alipokea ngao kutoka kwa Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohamed Kawaida iliyotolewa kwa azimio la UVCCM kuunga mkono na kutambua mchango na kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia kwa kipindi chake cha miaka mitatu madarakanI.

Akikabidhi tuzo hiyo kwa Makamu wa Rais mjini Kigoma Mwenyekiti huyo wa UVCCM amesema kuwa Rais Samia amefanya kazi kubwa ambayo haina mfano wa kupigiwa hivyo UVCCM imemkabidhi Sh milioni moja kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea urais kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.