MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IJP), Camillus Wambura kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa Jeshi la Polisi na kuwachukulia hatua askari wachache wanaoharibu taswira ya jeshi hilo.
Dk Mpango alitoa maagizo hayo jana ofisini kwake Dar es Salaam alipokutana na kuzungumza na IJP Wambura. Aliliagiza Jeshi la Polisi litende haki bila kuonea mtu na yeyote anayevunja sheria achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo.
Dk Mpango alilipongeza jeshi hilo kwa kuendelea kuimarisha amani na ulinzi wa wananchi na mali zao. Alisema kazi ya kulinda raia na mali zao ni msingi wa maendeleo ya nchi hivyo Jeshi la Polisi linapaswa kuhakikisha kunakuwa na utulivu wakati wote.
IJP Wambura alikwenda ofisini kwa Makamu wa Rais kujitambulisha zikiwa zimepita siku kadhaa tangu Rais Samia Suluhu Hassan amteue na kumuapisha kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi akichukua nafasi ya Simon Sirro ambaye sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.
Wakati Rais Samia akimuapisha IJP Wambura Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, alimweleza kuwa anataka mabadiliko na ufanisi. Rais Samia alimtaka IJP Wambura aimarishe usalama wa raia na mali zao, akisema alifanya vizuri akiwa Mkurugenzi Makosa ya Jinai (DCI) hivyo anatarajia atafanya vizuri zaidi akiwa Mkuu wa Jeshi la Polisi.