Mpango jumuishi kutatua changamoto sekta ya afya

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza na wananchi waishio kwenye mpaka usio rasmi wa Kashenye na Nangoma, ambao unamuingiliano mkubwa wa wananchi wa Uganda na Tanzania.

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii unalenga kutatua changamoto zilizopo katika sekta ya afya ikiwemo kupunguza mzigo kwa watumishi wa vituo vya afya na hospitali nchini.

Mwalimu ameyasema hayo leo wakati wa Uzinduzi wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

“Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii ndio askari wa mbele katika Sekta ya Afya kwa kuwa ndio wanaibua magonjwa na wanaweza wakazuia na kutoa taarifa zozote kuhusu masuala ya magonjwa, lakini pia ni nguzo muhimu katika kuimarisha mifumo ya Afya ili kufikia lengo la huduma za Afya kwa wote,” amesema kiongozi huyo.

Advertisement

Amesema wahudumu wa afya ngazi ya jamii wanapaswa kutoka kwenye jamii zao.

“…Sio mtu unatoka Tanga unaenda kufanya kazi Buhigwe kama mhudumu wa afya ngazi ya jami wakati Buhigwe wana mila zao wana taratibu zao na desturi zao za kuhudumia mgonjwa na kusaidia jamii,” amesema Ummy.

Amesema, wahudumu wa afya ngazi ya jamii watachaguliwa kupitia mikutano mikuu ya vijiji au watapeleka maombi kwenye vijiji au mitaa ndio vitawapitisha.

“Tunaamini hakutakuwa na vitendo vya rushwa wala upendeleo na tumewawekea malengo, watapitia angalau kaya 23 kwa wiki sawa na kaya 100 kwa mwezi pamoja na maeneo mengine yenye mkusanyiko kama masoko stendi za mabasi, nyumba za ibada na mikutano.

Wahudumu hawa watawajibika katika kituo cha kutoa huduma kilichopo katika eneo lake.

” Amesisitiza Waziri huyo.