SERIKALI imezindua Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, ambao utatoa ajira 137,294 Tanzania Bara kwa kada hiyo katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka huu.
Akizundua mpango huo jana Dar es Salaam, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema serikali inatambua umuhimu wa kada hiyo katika jamii na ndio maana imezindua mpango huo jumuishi wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
Alisema katika mpango huo, jumla ya ajira 137,294 za kada hiyo zitatolewa kuanzia mwaka wa fedha 2023/24 hadi 2027/28 na kuwa kwa mwaka wa kwanza jumla ya ajira 28,000 zitatangazwa na kisha zitaendelea kutangazwa kwa awamu ambapo kila mwaka unaofuata zitatangazwa ajira mpya 27,324.
Katika mpango huo serikali itatumia Sh bilioni 899.473kutekeleza mango huo kwa miaka mitano na katika mwaka wa kwanza, jumla ya Sh bilioni 99.67 zitatumika.
“Katika ajira hizi wahusika watachaguliwa kutoka katika maeneo yao, kila mtaa utakuwa na wahudumu wa afya ngazi ya jamii wawili, mmoja wa kike na mwingine mwanaume . Nitoe wito kwa wananchi wote wenye sifa wachangamkie fursa hii kwenye maeneo yao,’’alisema Dk Mpango.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan aliweka msukumo mkubwa na kuridhia programu hiyo kuanza kufanya kazi mara moja kutokana na umuhimu wake katika jamii.
Dk Mpango alisema huduma kuu nne kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ni kutoa elimu ya afya, huduma za afya kinga, huduma tembezi na mkoba na baadhi ya huduma za awali za tiba kabla ya kutoa rufaa.
Alisema pamoja na kkuchangua utatuzi wa changamoto za sekta ya afya nchini, mango mhuo umeweka kipaumbele kwenye huduma za lishe, afya ya mama na mtoto,vijana na uzazi wa mpango, magonjwa ya kuambukiza, malaria,Kifua kikuu, Ukimwi na magonjwa yasiyoambukiza, magonjwa ya mlipuko na dharura na masuala ya ustawi za jamii.
Aidha utekelezaji wa mpango huo utazingatia kanuni na miongozo hiyo hivyo na kuelekeza viongozi wanaohusika katika ngazi zote kuhakikisha wanachagua wahusika kwa kutumia kanuni, sifa na vigezo vilivyowekwa ili kupata wahudumu wenye sifa stahiki kutekeleza majukumu hayo.
“Kwa wahudumu watakaopewa jukumu hili , wajiepushe na upendeleo,rushwa na ukiukwaji wa taratibu, katika kutekeleza utaratibu huu,”alisema Dk Mpango.