Mpango kufungua shimmuta Tanga
MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango anatarajia kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mashindano ya Mashirika ya Umma, Makampuni na Taasisi Binafsi (Shimmuta) Novemba 21 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Hayo yalibainishwa jana na Mwenyekiti wa Shimmuta Taifa, Roselyne Massam wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa kuhusu mashindano hayo, ambapo alisema kwa mara ya kwanza tokea yalipoanza mwaka huu 2022 yameweka rekodi mpya.
Alisema rekodi hiyo inatokana na kuongezeka kwa idadi ya timu na sasa kufikia 52 zitakazochuana katika kuwasaka mabingwa kupitia michezo watakayoshindaniwa ambayo ilianza juzi.
Mwenyekiti huyo alisema tangu wameshika hatamu ya kuliongoza shirikisho hilo haijawahi kutokea kushirikisha timu nyingi zaidi kama mwaka huu jambo ambalo linaonesha mwitikio kuwa mkubwa na michezo hiyo.
Naye Mratibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Maswet Masinde alisema kuwa awamu hii wamejipanga hakuna mamluki atakayechezeshwa kwenye timu zitakazoshiriki mashindano hayo kwani watahakikisha wanasimamia sheria, kanuni na taratibu zinazowaongoza katika michezo yote.
Mratibu huyo alisema kuwa tayari wanamichezo 2,183 wako jijini hapa kushiriki mashindano hayo.
Michezo itakayochezwa katika mashindano hayo ni michezo ya mpira wa miguu kwa wanaume, mpira wa pete, wavu, kikapu, dats, pool table, vishale, drafti, kukimbia kwa magunia, riadha, kuvuta kamba, bao na mingineyo, lengo kuu likiwa kuimarisha uhusiano na kuimarisha afya za wafanyakazi kupitia michezo.



