Mpango mkakati chakula cha wanafunzi Katavi waja

MKUU  wa Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi Onesmo Buswelu amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tanganyika kuhakikisha anaanda mpango mkakati wa namna suala la wanafunzi kupata chakula shuleni litatekelezwa kuanzia Januari hadi Disemba 2023.

Buswelu ametoa agizo hilo katika kikao cha ushauri wa wilaya (DDC) kilichofanyika katika ukumbi wa Mkurugenzi Tanganyika.

Aidha, amewataka watendaji wa Kata kulisimamia hilo kwa ukamilifu kuhakikisha wazazi wanatoa michango ya vyakula ili kuwawezesha watoto wao kutoshinda njaa wawapo shuleni.

Advertisement

“Faida ya kula chakula cha mchana wakiwa shuleni,inawezesha kwanza watoto kutengeneza umoja na mshikamano, ‘social life’ inaanzia pale shuleni kwa hiyo watendaji wa Kata tutapita na tukifika cha kwanza tupate taarifa ya namna gani mnafanya ili watoto wapate chakula”

Amesema haoni sababu kwa wazazi kushindwa kuchangia vyakula kwa ajili ya watoto wao ukilinganisha Wilaya hiyo inazalisha mazao kwa wingi na vyakula ni vya kutosha.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Wilaya hiyo Betuely Ruhega amesema wameweka mikakati sita ya kuhakikisha chakula kinapatikana shuleni.

Ruhega amesema mkakati mmoja wapo ni pamoja na kutoa elimu kwa kamati na bodi za shule,serikali za vijiji kutunga sheria ndogo za kuwabana wazazi kutoa ushirikiano, shule kuanzisha bustani na mashamba ya chakula, kuhamasisha upandaji miti ya matunda, kuongea na wadau kuchangia chakula sanjari na kuendelea kuwahamasisha wazazi.

Mnamo Oktoba 29, 2021 Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilizindua mwongozo wa Kitaifa wa Utoaji huduma ya chakula na Lishe kwa wanafunzi wa Elimu msingi wenye lengo la kuwaelekeza wadau wa elimu nchini namna bora ya kutekeleza utoaji huduma ya chakula na lishe kwa wanafunzi.

Mwongozo huo ulizinduliwa jijini Dodoma na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Leonard Akwilapo ambapo alisema Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 imetamka wazi kuwa utoaji wa huduma muhimu kama chakula bora, maji safi na upatikanaji wa huduma za afya kwa wanafunzi wawapo shuleni ni muhimu. Hivyo Wizara imeandaa Mwongozo wa kisera ili kuweka utaratibu wa Kitaifa utakaonufaisha shule na wanafunzi wote wa Elimu msingi nchini.