Mpango: NAM tushirikiane biashara, majanga

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amehimiza Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) ziendelee kuongeza ukuaji wa kiuchumi kwa kushirikiana katika biashara na uwekezaji.

Aidha, amesema ushirikiano wa nchi hizo utaongeza ufanisi kukabili majanga kwa sababu janga la Covid-19 limetoa funzo kuwa hakuna nchi inayoweza kukabili majanga peke yake. Alisema hayo katika mji mkuu wa Azerbaijan, Baku kwenye mkutano wa NAM kuhusu namna ya kupambana na athari za Covid-19, akisema ushirikiano wa kiuchumi utarahisisha mapambano ya athari za janga hilo.

Dk Mpango alisema Tanzania imejifunza kuwa katika kupambana na changamoto za Covid-19, ushirikiano baina ya mataifa ya NAM ndio nguzo pekee ya ushindi na kwamba kamwe hakuna taifa linaloweza kushinda changamoto kama hiyo kwa kukabiliana nazo kivyake.

Alisema ili mataifa ya NAM yawe na uwezo wa haraka wa kukabili changamoto za majanga, ni lazima yaimarishe tafiti za maendeleo zitakazosaidia nchi kupata suluhu ya mambo yatakayosibu nchi. “Kila nchi ihakikishe inaongeza utafiti wa bioteknolojia itakayowezesha kuwa na dawa za maradhi mbalimbali, uzalishaji wa chanjo pamoja na vifaa tiba,” aliongeza Makamu wa Rais katika hotuba yake.

Alihimiza nchi hizo ziongeze uwezo wa kupambana na majanga kwa kuimarisha miundombinu ya kuwezesha kukabili majanga ikiwamo kuimarisha mifumo ya afya, kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya pamoja na kuimarisha sera ya lishe bora kwa wananchi. Aliueleza mkutano huo kuwa katika kukabili athari za Covid-19, Tanzania imefanikiwa kwa kuongezeka Pato Ghafi la Taifa (GDP) hadi kufika asilimia 5.

2 mwaka 2022 kutoka asilimia 4.

2 mwaka 2021.

Alisema Tanzania ilipata mafanikio hayo kwa kutekeleza maelekezo ya afya ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu namna ya kukabili changamoto hiyo kwa kusambaza chanjo kwa wakati.

Pia alisema Tanzania ilifanikiwa kuwezesha na kusambaza vifaa wezeshi kupambana na janga hilo pamoja na kuandaa wataalamu kwa kuwapa mafunzo ya namna ya kukabiliana nalo bila kuhatarisha maisha yao.

Alisema Serikali ya Tanzania iliandaa na kutekeleza mpango kukabiliana na athari za Covid-19 kwa kutumia mkopo wa riba nafuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuimarisha sekta za afya, maji, utalii na usafirishaji.

Dk Mpango aliziomba nchi zenye nguvu hususani nchi za Magharibi kuziondolea vikwazo vya kiuchumi nchi wanachama wa NAM za Cuba na Zimbabwe kwa sababu uwepo wa vikwazo hivyo unaumiza wananchi wa nchi hizo na kurudisha nyuma shughuli za maendeleo.

Rais wa Azerbaijan anatarajiwa kukabidhi kiti cha uenyekiti wa NAM kwa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na Dk Mpango aliihakikishia Uganda ushirikiano wa kutosha kutoka Tanzania.

Habari Zifananazo

Back to top button