Mpango: Uongozi kazi ngumu, tuombeeni

Dk Mpango.

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema kuongoza ni kazi ngumu hivyo ameomba wananchi waendelee kuwaombea viongozi ili waongoze taifa kadri inavyompendeza Mungu.

Dk Mpango alisema hayo Dodoma jana asubuhi wakati akiwasalimu waumini wakati wa Ibada ya Jumapili katika nyumba ya malezi ya Mtakatifu Yosefu iliyopo Miyuji.

“Tunahitaji sana msaada wa Mungu, kwa hiyo nawaomba mtuombee ili tuongoze taifa hili inavyompendeza Mungu mwenyewe. Muiombee nchi iendelee kukaa na amani, mtuombee na sisi watumishi wa taifa hili kwa upande wa serikali tuweze kuenenda ipampasavyo Mungu,” alisema.

Advertisement

Dk Mpango alisema mienendo katika taifa hivi sasa haimpendezi Mungu, maadili yameporomoka hivyo wazazi na walimu wazingatie suala la malezo ya watoto.

Alisema ni vema wazazi waache kulalamika, wafanye kazi ya ziada kufuatilia mienendo ya watoto.

“Mienendo ya vijana hata waliopo vyuoni ni muhimu sana, sana, sana, turekebishe maadili, tumekosea,” alisema Dk Mpango.

Alitoa mwito kwa waumini wa kanisa hilo na wananchi wa Dodoma waongeze jitihada katika usafi wa mazingira, wapande miti ya kivuli, matunda, maua na waepuke tabia za kutupa takataka ovyo.

Dk Mpango alisema Mwenyezi Mungu ameijaalia Tanzania mazingira mazuri hivyo ni muhimu kuyatunza kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *