KIGOMA: MKOA wa Kigoma unaelezwa kupiga hatua kubwa katika kukabiliana na vifo vya mama wajawazito na watoto wakati wa kujifungua, ambapo hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali kwa kushirikiana na wadau zimetajwa kufanikisha jambo hilo.
Akizungumza na vyombo vya habari, katika Kituo cha Afya Kiganamo Halmashauri ya mji wa Kasulu, mhamasishaji jamii wa Shirika la Thamini Uhai, Ignus Kalongola amesema kuwa moja ya mafanikio makubwa ya jambo hilo ni uwepo wa huduma ya msindikizaji wa mama mjamazito.
Kalongola amesema kuwa mpango unaotekelezwa kwa mama mjamzito ni kuwa na msindikizaji tangu anapoanza kwenda kliniki hadi siku ya kujifungua, huku msindikizaji huyo akiruhusiwa kuwepo karibu na mama mjamzito hadi wakati wa kujifungua.
Joseph Jackson, ni mmoja wa wasindikizaji kwa mwenza wake ambaye anasema amehamasika kumsindikiza mke wake tangu alipoanza kliniki ya ujauzito hadi kujifungua, na sasa wanaongozana pia kliniki ya mtoto ili aweze kufuatilia kwa ukaribu maendeleo ya afya ya mke wake na mtoto.
Msindikizaji huyo amesema mpango huo umemuwezesha kujua mambo mengi kuhusiana na masuala ya afya ya uzazi, na anaweza kumsaidia mama mjamzito mahali popote huku akiwaomba wanaume wengi kulifuata.
Muuguzi wa kituo hicho, Tecla Masanja amesema kwa sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la mama wajawazito wanaofika kujifungua jambo lilichongiwa na kuwepo kwa mpango wa mama wajawazito kuongozana na msindikizaji wake.
Kwa sasa kituo hicho kinazalisha hadi mama wajawazito 500 kwa mwezi kuanzia mwaka 2019, ukilinganisha na wastani wa mama wajawazito 200 waliokuwa wakijifungua wakati huo.