Mpango: Walioiba fedha za umma watakiona

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema kukithiri kwa wizi wa fedha za umma ni ishara ya mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Dk Mpango alisema hayo wakati yeye na mkewe, Mbonimpaye Mpango walipoungana na waumini katika ibada ya asubuhi katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Fransisco Nzavery – Nyakahoja jijini Mwanza.

Katika ibada hiyo iliyoongozwa na Padri Victor Awiti, aliwasihi Wakristo na Watanzania kwa ujumla hasa wazazi wajitafakari kukabili mmomonyoko wa maadili.

“Lakini ikiwa nafasi nyingine, walimu tunavyowaongoza wanafunzi wetu wa ngazi zote kuanzia shule za awali, shule za msingi, sekondari, vyuo, hata vyuo vikuu. Lazima tuangalie tena mfumo mzima kama wazazi kwa hakika kuna sehemu tumeteleza…lazima tujitafakari tena tumrudie Mungu,” alisema Dk Mpango.

Awali wakati anazungumza na wananchi wa Wilaya ya Kwimba akiwa eneo la Hungumalwa mkoani Mwanza, alisema serikali itawachukulia hatua wote waliotajwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wakibainika wamefanya ubadhirifu wa fedha za umma.

Dk Mpango alisema kila kiongozi anapaswa kuhakikisha fedha zinazopelekwa katika eneo lake zinatumika kama ilivyokusudiwa.

“Tumeanza kuwachukulia hatua viongozi wote ambao wanathibitika kwenye taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, hao waliokula fedha zenu watapata cha moto.

“Kwa hiyo viongozi nawaasa tena mhakikishe fedha zinazokuja Kwimba, zinazokuja katika Mkoa wa Mwanza, zinazokuja katika mikoa mingine yote ya nchi yetu zinasimamiwa ipasavyo na asiwepo mtu wa kudokoa hizo fedha,” alisema.

Alihimiza wananchi katika eneo hilo waitunze miradi inayopelekwa na serikali ili idumu kwa muda mrefu.

Aidha, aliwasihi kujikita katika ufugaji wenye tija na utakaowapa matokeo ya haraka ili kukabili uharibifu wa mazingira unaotokana na ufugaji wa kuhamahama.

Akiwa wilayani Misungwi, Dk Mpango alihimiza wananchi walinde na kudumisha amani sanjari na kuzingatia maadili ya Kitanzania kwa kuwalinda watoto dhidi ya maudhui yasiyofaa kwenye televisheni.

Jana, Dk Mpango alitembelea Manispaa ya Ilemela kujionea shughuli za maendeleo akaihimiza jamii iwe karibu na watoto kuwalinda na kulinda utamaduni, mila na desturi za Mtanzania.

Alisema ni muhimu kuwa karibu na watoto ili kubaini matukio ambayo yasipodhibitiwa yanaweza kuharibu malezi katika jamii.

Habari Zifananazo

Back to top button