Mpogolo: ‘Machinga’ zingatieni maelekezo

DAR ES SALAAM: MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewataka wafanyabiashara wadogo ‘Machinga’ waliopo Kariakoo kuzingatia maelekezo yanayotolewa na serikali ili kuhakikisha uendeshaji wa soko hilo unakuwa na ufanisi na kuinufaisha serikali na wafanyabiashara kwa ujumla.

Mpogolo anaysema hayo baada kufanyikan kwa tathimini ya mwenendo wa kibiashara katika soko hilo na kubaini kuwapo kwa changamoto kadhaa ambazo hukwamisha malengo ya serikali ikiwemo kukusanya mapato ambayo hutumika kwa ajili ya huduma mbali za kijamii.

Mpogolo anayaesema hayo mbele ya waandishi wa habari akiwa na wawakilishi wa kundi hilo la wafanyabiashara , amesema wao wana jukumu la kufanya Soko la Kariakoo liendelee kuwa la kimataifa kwani ni eneo muhimu kwa uchumi wa nchi na ambalo limetoa fursa za ajira kwa Watanzania wengi.

Advertisement

Amezitaja baadhi ya changamoto walizobaini ni pamoja na kuwapo kwa meza na miamvuli kwa wafanyabiashara ndogondogo ambao wamerudi katika baadhi ya maeneo ambayo awali walizuiwa.

“Miamvuli inazuia huduma zingine katika maduka na wengine kuonekana wanakwepa kodi na wengine kushindwa kufanya biashara.

“Kuna baadhi ya wafanyabaishara wenye maduka wametumia nafasi hiyo kutapisha mizigo, mtu ana bodaboda unakuta amezitoa zote kwenye eneo ambalo watu wanapita kwa miguu. Baadhi ya maduka wametoa sanamu za midoli wameweka barabarani na wanaouza friji wanazitoa wanaweka barabarani hali kadhalika wanaouza magodoro,” amesema Mpogolo.

Amesema hali hiyo imekuwa kero kwa watumiaji wengine wa barabara wakiwemo watembea kwa miguu huku Mamlaka ya Mapato (TRA) nayo ikishindwa kujua wakati gani bidhaa zimeuzwa.

“Baadhi ya wafanyabiashara wenye maduka marobota wanaweka katikati ya barabara na kusababisha zisitumike kama ilivyokusudiwa. Maegesho ya magari na bajaji ni changamoto mtu anaweza akaegesha mbele ya duka au eneo ambalo halistahili.

“Matangazo yanaendelea kila mtaa kuhakikisha kila mfanyabiashara amepata taarifa, wale wanaotoa mizigo nje tayari tumewapelekea notisi na endapo watakiuka sheria itachukua mkondo wake…tunataka kufanya Kariakoo iendelee kuwa soko la kimataifa na la kisasa,” amesema.

Amesema pia wanaendelea na maboresho katika soko hilo kuhakikisha linafanya kazi kwa saa 24 ambapo wameshaanza kufunga taa katika Mitaa ya Mchikichini, Mkunguni, na Tandamti sambamba na kufunga kamera kudhibiti usalama.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Martine Mbwana, amekiri kuwapo kwa changamoto hizo na kuahidi kutoa ushirikiano kuhakikisha hadhi ya soko hilo inaendelea kuwepo.

Mwenyekiti wa Wamachinga Kariakoo, Stephen Lusinde, ameshukuru kushirikishwa katika zoezi hilo kubaini changamoto hizo ambapo wamekubaliana kuzitatua kwa pamoja.

“Changamoto kweli zipo hasa sisi wafanyabiashara wadogo kuna baadhi ya maeneo tumeziba mitaa, kuanzia kesho (Machi 28) tutaanza kurekebisha maeneo yetu kuhakikisha tunakwenda sambamba na wafanyabishara wenzetu na wenye maduka,” amesema Lusinde.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Jomaary Satura, amesema wamewashirikisha wafanyabiashara katika kufanya tathmini hiyo ili soko hilo liendelee kuwa na ufanisi.

“Tumeona tusipochukua hatua uendeshaji wa soko hautakuwa na ufanisi, tunataka lifanye shughuli zake kwa ufanisi wa hali ya juu ili kila mmoja aweze kunufaika na uwepo wa Soko la Kariakoo,” amesema Satura.

Wafanyabashara warudi kwenye maeneo waliyopangwa, watumie meza na miamvuli kama walivyokubaliana awali.

Eneo ambalo halijapangwa ni marufuku kwa mfanyabishara ndogondogo kwenda kufanya biashara.

Wafanyabiashara wa maduka kila mmoja arudishe bidhaa zake ndani ya duka na si kutapisha nje na yeyote akatayekiuka atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Kwenye barabara za mwendokasi na maeneo mengine ya huduma za kijamii hawatakiwi kwenda.

Wenye bajaji na magari ya mizigo watatafutiwa eneo la kuegesha.