SERIKALI imeanza kutekeleza mradi wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro litakalogharimu Sh bilioni 335 ambalo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji yatakayotumika kwa miaka mitatu mfululizo.
Ujenzi huo unasimamiwa na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa).
Hayo yalisemwa na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Kiula Kingu, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Morogoro.
Alisema lengo la utekelezaji mradi huo ni kuwezesha mitambo ya maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini kuwa na maji ya kutosha ili kuzalisha maji kipindi cha kiangazi.
Aidha, Kingu alibainisha kuwa bwawa hilo litakapokamilika litakuwa linahifadhi maji kipindi cha masika ili maji hayo yaweze kutumika nyakati za kiangazi.
Kiula alieleza faida za mradi huo na namna utakavyotoa fursa mbalimbali kwa taifa ikiwemo ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 101, uzalishaji wa umeme megawati 20, uvuvi na utalii.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Grace Nsemwa, aliipongeza serikali kwa uthubutu wa utekelezaji wa mradi na kutoa wito kwa Dawasa kuusimamia na kuutekeleza mradi kikamilifu ili ulete manufaa kwa Watanzania.
“Tunajivunia utekelezaji wa mradi huu katika mkoa wetu wa Morogoro, Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa kipindi chote cha kiangazi kwa hiyo tuunge mkono juhudi hizi kwa kuhakikisha Dawasa wanatekeleza mradi huu kikamilifu kama ilivyo matarajio ya Watanzania,” alisisitiza.
Mkurugenzi wa Bonde la Wami Ruvu, Elibariki Mmasi, alielezea mikakati ya uhifadhi wa vyanzo vya maji kwa kuhakikisha vyanzo vyote vinavyoingia katika Bwawa la Kidunda vinakuwa na maji ya kutosha.
“Tumejipanga kufanya tathmini katika maeneo yote yanayozunguka chanzo cha Mto Ruvu na yatatangazwa kuwa maeneo ya uhifadhi kwa kutenga shilingi bilioni nne ili kuhakikisha Bwawa la Kidunda linatoa suluhisho la upatikanaji wa maji kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani,” alisema.
Mradi huo unatarajia kuanza rasmi Juni 18, 2023 na utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na kukamilika kwake kutapunguza matatizo ya maji kwa wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.