Mradi kutoa mafunzo kwa wajasiriamali
MRADI wa kukuza ajira na ujuzi kwa vijana Tanzania (E4D) unatoa mafunzo ya namna ya kupata zabuni katika miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na kampuni za nje ya nchi, lengo likiwa ni kuwezesha watanzania kushiriki na kushinda.
Ndani ya program hiyo jumla ya kampuni 300 za nchini wakiwemo wajasiriamali wadogo na wakati (SMEs) watashiriki kupewa mafunzo yatakayosaidia kupata ujuzi na kuongeza ajira kwa vijana walio wengi.
Naibu Kiongozi wa mradi, Denis Mbangula amesema hayo leo Dar es Salaam katika mafunzo yaliyowashirikisha kampuni za Kitanzania ili kuwajengea uwezo wa namna ya kuingiza katika zabuni za kampuni za nje ya nchi.
Amesema program hiyo inaratibiwa na serikali kwa pamoja na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) na kutekelezwa na E4D ambayo itawezesha kampuni za Tanzania kushindana katika zabuni zinazohusisha miradi mikubwa.
“Tunataka kampuni za Tanzania zishiriki na kushinda ili ziajiri vijana walio wengi nchini,” amesema Mbangula na kuongeza kuwa mradi umekuja kujaribu kusaidia serikali ya Tanzania ili kupunguza kero kwani miradi mingi inayokuja inatekelezwa na watu kutoka nje hivyo kampuni za ndani zitakuwa na uwezo mkubwa wa kushinda na kuajiri vijana.
Amesema katika mradi mambo ya jinsi ya kuandaa hizo zabuni zinafundishwa na kufikia vigezo vilivyotakiwa kwa kuwa ni muhimu kwa kampuni za Tanzania zishiriki na kushinda lakini pia kufundishwa suala la usalama kazini, ili kuweza kupata zabuni.
Amesema mradi ulianza Machi mwaka jana 2022 na mafunzo yataendelea hadi Agosti mwaka huu yakihusisha kampuni 300 za kitanzania kuleta wafanyakazi wake wawili kutoka kitengo cha zabuni hivyo jumla ya watu 600 wataweza kujifunza.
Ametoa wito kwa wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) kuwa na na uthubutu wa kuweza kushiriki katika kuomba zabuni wawe na moyo wa kutafuta taarifa pia watumie mafunzo hayo ili kutimiza vigezo vinavyotakiwa kwenye zabuni.
Mbangula amesema mradi unatekelezwa katika nchi sita ambazo ni pamoja na Kenya, Uganda Msumbiji, Afrika Kusini Ghana na Nigeria.
Kiongozi wa mradi huo, Kabongo Mbui amesema mradi huo pia unashirikisha sekta binafsi kupata ujuzi wa namna ya kupata zabuni za kampuni za nje zenye miradi mikubwa lengo likiwa ni kusaidia wajasiriamali wadogo na wakati kushiriki.
Akifungua mkutano huo,Mkurugenzi Idara ya Viwanda vidogo na kati katika Wizara ya Viwanda na Biashara, Wilfred Kahwa amesema suala la kupata zabuni kwa watanzania ni changamoto kubwa hususani kwa wajasiriamali wadogo na wakati.
Amesema kwa mafunzo hayo itasaidia SMEs kujua utaratibu mzima na kuweza kushiriki kwa kuwa zabuni za kampuni za nje ni fursa ya kuwaimarisha na kuwa na motisha wa kuboresha shughuli zao.