Mradi wa bil 65/- kupatia kaya 250 maji

WAKAZI wa Mtaa wa Nyakasangwe, Kata ya Wazo Kinondoni mkoani Dar es Salaam, wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama baada ya kutekelezwa kwa mradi mkubwa wa maji.

Mradi huo umetekelezwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (DAWASA) kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kupitia mradi wa kutoka Makongo hadi Bagamoyo.

Mhandisi wa miradi Mkoa wa kihuduma Dawasa Mivumoni, Pascal Salida, alisema mradi huo umegharimu Sh bilioni 65.4.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyakasangwe, Anthony Mwandege, alisema wananchi wengi hawakuwa na huduma ya majisafi na maeneo yao yalikuwa na changamoto ya msukumo mdogo wa maji lakini sasa changamoto hiyo haipo.

Alisema wananchi wa mtaa wake wana furaha kwa kuwa wataondokana na adha ya kutumia maji ya chumvi pamoja na kutumia gharama kubwa ya kununua maji kutoka kwa wafanyabiashara binafsi.

“Eneo kubwa la Nyakasangwe linapata maji kwa mara ya kwanza, jambo ambalo ni historia hapa kwetu, lakini hata kwa kipande kidogo kilichokuwa kikipata huduma kwa mgawo wa maji ambao haukuwa sawa, sasa huduma imeimarika na upatikanaji wa maji ni wa uhakika,” alisema.

Alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kuunganishiwa huduma ya maji na kuahidi kuwa serikali ya mtaa italinda miundombinu hiyo na kupambana na yeyote atakayethubutu kuiharibu.

“Kwa kushirikiana na Dawasa tutaweka mipango mizuri kwa pamoja ambayo kupitia hiyo kila mwananchi ataweza kulipia huduma ya majisafi kila mwezi kutokana na matumizi yake,” alisema Siwema Salum, ambaye ni mnufaika wa maji hayo.

Mkazi huyo alisema walikuwa wakitumia maji kutoka bwawani na hayakuwa salama kwa afya kwani pia mifugo ilikuwa ikiingia na kunywa maji  hayo. “Leo hii tunachota maji yanayotiririka bombani, hii kwetu ni kama ndoto, tunaishukuru sana serikali.”

Mhandisi wa miradi Mkoa wa kihuduma Dawasa Mivumoni, Salida, alisema kwa sasa kazi ya kuwaunganishia wananchi maji inaendelea na hakuna mwananchi atakayeachwa kupatiwa huduma ya majisafi.

Alisema katika mtaa huo, malengo yao ni kuzipatia maji kaya zaidi ya 250. Hadi sasa, kaya zaidi ya 80 zinapata huduma.

Alisema mradi wa kuboresha huduma ya maji kutoka Makongo hadi Bagamoyo unalenga kuboresha upatikanaji wa maji kwa wakazi 450,000 na umehusisha ujenzi wa matangi matatu yaliyopo Vikawe, Mbweni na Tegeta A. Matangi hayo yatakayotumika kupokea na kusambaza maji kwa wakazi hao, yana ujazo wa lita milioni tano kila moja.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button