SERIKALI imeishukuru Benki ya Dunia kwa kutoa mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 425 sawa na Sh bilioni 972 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema mradi huo unatekelezwa kupitia vyuo vikuu 14, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Tume ya Sayansi, Teknolojia (Costech) na taasisi tano za Wizara ya Fedha na Mipango.
Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaeleza chama kinavyotambua umuhimu wa sekta ya elimu na mchango wake katika ajenda ya maendeleo kwa kuandaa mtaji watu wenye uwezo wa kutumia fursa za rasilimali zilizopo kujiletea maendeleo na kuchangia katika jitihada za nchi kufikia uchumi wa kati uliojikita katika misingi ya viwanda.
Kwa mujibu wa ilani hiyo, chama kinaagiza kushirikiana na sekta binafsi, asasi za kiraia zikiwamo taasisi za dini katika kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu na ujuzi na kuimarisha idara na taasisi za udhibiti ubora ikiwemo Nacte, TCU na Idara ya Udhibiti Ubora kuhakikisha kiwango cha ubora wa elimu itolewayo nchini kinazingatiwa.
Profesa Mkenda alisema ubora na ujuzi ni lazima izingatiwe katika mradi huo kwa kuwa vyuo vikuu ili udahili utakapoongezeka usipoteze ubora katika vyuo hivyo.
Alisema mradi huo utagusa pia vyuo vikuu binafsi na kwamba dola za Marekani milioni 1.1 zimetengwa, hivyo vinapaswa kufuatilia vipate fedha hizo. Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Francis Michael aliwashukuru washirika wa maendeleo wanaoshirikiana na serikali kuboresha elimu na akasema mradi wa HEET unatekelezwa kwa miaka mitano kuanzia 2021 hadi 2026.
“Kupitia mradi huu serikali itatoa ruzuku kwa vyuo vikuu binafsi kwa ajili ya kusomesha wahadhiri katika masuala ya afya na tiba kutokana na mahitaji makubwa ya wataalamu katika sekta hiyo, lakini pia kama sehemu ya mkakati wa serikali ya kushirikisha vyuo vikuu binafsi katika kuendeleza sekta ya elimu ya juu nchini,” alisema Dk Michael.
Aliongeza: “Kupitia utekelezaji wa mradi wa HEET, serikali itaboresha mazingira ya kufundishia na kujifunza katika vyuo vikuu na taasisi nufaika kwa kutekeleza masuala mbalimbali.” Alitaja maeneo yatakayoguswa na mradi huo kuwa ni ujenzi na ukarabati wa miundombinu kwa ajili ya matumizi ya kitaaluma na kiutawala.
Dk Michael alisema dola za Marekani milioni 329 sawa na Sh bilioni 753.5 zitatumika kujenga miundombinu mipya na kukarabati iliyopo zikiwamo kumbi za mihadhara na madarasa 130, maabara na karakana 108, mabweni 34, ofisi 23 na miundombinu ya mashamba na vituo atamizi 10.
Alisema pia vitawekwa vifaa vya kisasa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika vyuo vikuu na taasisi nufaika za mradi. Uboreshaji huo utaongeza udahili katika programu za kipaumbele kutoka wanafunzi 40,000 mwaka 2020 hadi kufikia wanafunzi 106,000 mwaka 2026.
Pia alisema serikali itajenga kampasi mpya 14 katika mikoa ya Lindi, Katavi, Rukwa, Mwanza, Tanga, Shinyanga, Kigoma, Simiyu, Ruvuma, Singida, Tabora, Manyara, Kagera na Dodoma.
“Kwa Mkoa wa Dodoma, serikali itajenga chuo kikuu cha kisasa cha tehama, bila shaka mtakumbuka ujenzi wa chuo hicho ni sehemu ya ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema.
Dk Michael alisema eneo lingine ni uboreshaji wa baadhi ya mitaala na uandaaji wa mitaala mipya ya programu za vipaumbele ili iendane na mahitaji ya soko la ajira kwa sasa. Alisema dola za Marekani milioni 7.97 sawa na Sh bilioni 18.23 zitatumika kuhuisha na kuandaa mitaala mipya zaidi ya 290 kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa inaendana na kujibu mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Pia Dk Michael alisema serikali itatumia dola za Marekani milioni 7.79 sawa na Sh bilioni 17.93 kuboresha mazingira ya kubuni, kuunda teknolojia na kuziendeleza ili kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.
Alisema mradi huo utasomesha wanataaluma kuanzia ngazi ya shahada ya umahiri hadi uzamivu na kutoa mafunzo kazini kwa watumishi. Dk Michael alisema mradi huo unalenga kusomesha takribani wahadhiri 1,100 wakiwamo 623 katika shahada ya uzamivu, wahadhiri 477 katika shahada za umahiri.
Alisema wahadhiri na watumishi wengine katika vyuo vikuu, wizara na taasisi nyingine watakuwa wanufaika wa mradi kwa kupata mafunzo ya muda mfupi na viwandani ndani na nje ya nchi.
Alisema katika kutambua mchango wa sekta binafsi, serikali itatumia sehemu ya fedha za mradi kufadhili masomo kwa wahadhiri wa vyuo vikuu binafsi na kutoa mafunzo katika fani za afya na tiba.
Mratibu wa mradi huo, Dk Kennedy Hosea alisema HEET una lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na mitaala yaendane na mahitaji ya soko la ajira.
Dk Hosea alisema mradi una vipaumbele 14 ambavyo ni uhandisi na teknolojia, Tehama, sayansi, sayansi ya afya na tiba, mipango miji, mazingira na teknolojia, nishati jadidifu, rasilimali maji, mabadiliko ya tabianchi, kilimo na biashara, hifadhi ya wanyamapori, utalii na ukarimu, taaluma ya viwanda na ualimu.