‘Mradi wa EACOP utanufaisha wote’

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema mradi wa bomba la mafuta ghafi (EACOP) utanufaisha Watanzania wote.

Amesema amasikitishwa na baadhi ya Watanzania kujiunga na watu wa nje na kuunda kampuni feki, ambazo nia yake ni kujiingiza kwenye mradi huo kwa njia isiyo halali na kueleza kuwa tayari jambo hilo limesimamiwa vyema na Mamlaka ya Udhibiti wa Mafuta na Maji (Ewura).

Dk Biteko amesema hayo leo alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kuweka mifumo ya kupasha na kuzuia upotevu wa joto kwenye bomba la mafuta lililopo Kijiji cha Sojo,Nzega mkoani Tabora, bomba linalotoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani Tanga nchini Tanzania.

Advertisement

Amesema amemueleza Mkurugenzi Mkuu wa EACOP, kuhakikisha wanatumia kampuni za Watanzania kwanza na zinazoeleweka, huku akiwataka Watanzania wautunze mradi huo na kusaidia katika ulinzi na usalama.

Dk Biteko pia amesaini mikataba mitatu, ambapo mkataba wa kwanza ni kukodisha miundombinu ya eneo la kuhifadhi mafuta, mkataba wa pili kutumia maji na mkataba wa tatu kutumia shughuli za bandarini.

Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), Mussa Makame, amesema wao ni wana hisa wanatekeleza majukumu yao, wanatakiwa kuchangia hisa ya Sh bilioni 820, lakini mpaka sasa wamechangia Sh bilioni 710 sawa na asilimia 87 na kushirikiana na EACOP kuhakikisha ardhi inapatikana kwa ajili ya kuweka kiwanda hicho.

Mkurugenzi Mkuu wa EACOP, Martin Tiffen amesema wanayo furaha kuanzishwa kwa karakana hiyo, ambayo ni hatua muhimu katika kujenga miundombinu itakayosafirisha mafuta salama.