Mradi wa Maji Butimba kukamilika Julai, 2023

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa), Christopher Gachuma, ameikaikishia kamati ya uwekezaji na mitaji ya umma (PIC) kukamilika kwa mradi wa maji Butimba, mwezi Julai mwaka huu.

Amesema wakati wa ziara ya PIC kwenye mradi huo kwamba, kazi zote zinazohusisha zege zimeshakamilika kwa takribani asilimia 80, huku manunuzi ya mitambo ya kusukuma majisafi kwenda baadhi ya matengi ikiwa imewasili kwenye mradi.

Kadhalika, manunuzi ya vifaa vya kieletrokini na umeme yameshafanyika na vinatarajiwa kuingia nchini wakati wowote kuanzia leo (mwishoni mwa Machi).

Advertisement

“Kwa ujumla, ujenzi wa mradi wote umefikia asilimia 71 na unatarajiwa kuanza majaribio mwezi Mei,” amesema.

Amekiri mradi huo ambao ujenzi wake ulianza mwezi Februari, 2021, kuwa nyuma ya muda kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo kuongezeka kwa kazi kama vile kuupa uwezo wa kuzalisha lita millioni 48, kutoka lita millioni 40 kwa siku.

Ongezeko hilo lilihusisha pia kupanuliwa kwa bomba na dakio la maji kutoka Ziwa Victoria, ambapo ndio chanzo cha mradi, ili kuzalisha maji lita millioni  96 kutoka  millioni  48 kwa siku.

Vilevile, mradi huo wenye thamani zaidi ya Sh65 billioni, ulichelewa kuanza kwa zaidi ya miezi minne, kutokana na kuchelewa kwa kibali cha msamaha wa kodi ili mkandarasi aweze kununua vifaa.

Kaimu Mwenyekiti PIC, Vuma Agustono, ameeleza kudhirishwa na maendeleo ya mradi, akasistiza umuhimu wa kuukamilisha kwa muda uliopangwa, ili kuondoa adha ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Mwanza.

/* */