Mradi wa Maji Butimba sasa kukamilika Desemba

Mradi wa Maji Butimba sasa kukamilika Desemba

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ameipongeza Wizara ya Maji kwa kutekeleza agizo la kuhakikisha Mradi wa Maji Butimba, uliopaswa kukamilika Februari mwakani unakamilika Desemba mwaka huu.

Dk Mpango alitoa agizo hilo Jumanne jijini Mwanza alipozindua Kituo cha Mabasi Nyamhongolo na wananchi wakamlilia kuhusu ukosefu wa maji safi na salama.

“Baada ya kusikia sauti za wananchi zimekuwa nyingi kuhusu uhaba wa maji, nikamuagiza Waziri wa Maji na kamati yake aliyoambatana nayo wajadiliane na mkandarasi kuona ni jinsi gani mradi huu unaweza kukamilika mapema zaidi,” alisema Dk Mpango.

Advertisement

“Nashukuru hili limetekelezwa na wananchi nawaahidi kwamba hii itakuwa zawadi yenu ya Krismasi kutoka kwa mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema jana katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la mradi huo.

Aliziagiza pia mamlaka husika kuwapa kipaumbele wananchi walio jirani na mradi huo, lakini pia kuwaunganishia wanufaika wote maji majumbani mwao kwa muda uliopangwa, ambao si zaidi ya siku saba kwa kila mwombaji.

“Haiwezekani wakazi wa Mwanza wakapata shida ya maji wakati Ziwa Victoria lipo hapo ambalo ni kubwa kuliko yote barani Afrika. Na pia msiwabambikie wananchi ankara za maji,” aliagiza Dk Mpango.

Alisema serikali inaendelea kuboresha huduma za maji nchi nzima ili kuhakikisha lengo linafikiwa, ambalo ni asilimia 95 ya upatikanaji wa maji maeneo ya mijini na asilimia 85 vijijini ifikapo mwaka 2025.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema utekelezaji wa Mradi wa Maji Butimba utafanyika usiku na mchana ili kutimiza ahadi ya upatikanaji wa maji ifikapo Desemba.

Aweso alisema kukamilika kwa mradi huo kutapunguza uhaba wa huduma za maji mkoani hapa kwani utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 48 kwa siku.

Alisema mahitaji ya maji kwa Mkoa wa Mwanza ni lita milioni 160 na uzalishaji wa sasa ni milioni 90 tu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Anthon Sanga alisema mradi utaisha kama wizara ilivyokubaliana na tayari kazi zote zinazohusu zege zimekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na zimebaki za umeme tu.