Mradi wa maji Kemondo wafikia asilimia 87

Mradi wa maji Kemondo wafikia asilimia 87

MRADI wa maji wa Kemondo-Maruku unaotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), umefikia asilimia 87 kwa awamu ya kwanza.

Mradi huo unatarajia kutekelezwa kwa awamu mbalimbali na kuhudumia  vijiji 17 katika Halmashauri ya Bukoba na Muleba.

Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Bukoba, Mhandisi Evarsto Mgaya, akitoa taarifa kwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Nadhifa Kemikimba mwishoni mwa wiki alisema awamu ya kwanza ukikamilika utahudumia wananchi 17,500, Kata ya Kemondo.

Advertisement

Amesema utaendelea kutekelezwa kwa awamu hadi kuzifikia kata zote za Maruku, Kanyangereko, Bujugo, Katerero, zilizoko Wilaya ya Bukoba na Kata ya Muhutwe iliyoko Wilaya ya Muleba.

Alisema upande wa Halmashauri ya Bukoba, upatikanaji wa maji safi na salama ni asilimia 74 na Ruwasa inataka hadi mwaka 2025 upatikanaji wa maji vijijini iwe asilimia 85 kulingana na Ilani ya CCM.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu alisema awamu ya kwanza isizidi Aprili mwaka huu, kwani kumekuwepo na uchelewashaji kutokana na wakandarasi kutofuata maagizo, ingawa serikali iliwaondoa kazini na kuweka wapya.

“Watendaji tusisubiri mwaka 2025 ndo tufikie asilimia 85, hapana tunataka mwaka 2024 tufikie asilimia hiyo na mwaka 2025 tuangazie ukarabati au mapungufu yaliyopo yarekebishwe.

“Lengo la serikali ni kila kijii kila mwananchi kupata maji safi na salama na hakuna atakayeachwa,”alisema Kemikimba.

Katika ziara hiyo amekagua na kutembelea miradi ya maji ya Ruzinga wilayani Missenyi na mradi wa Maji wa Kyamihorwa Wilaya ya Muleba, ambapo amewataka Ruwasa kuhakikisha wanawasimamia wakandarasi, ili miradi hiyo ikamilike haraka na kuwanufaisha wanachi.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *