WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Mtwara, inatarajia kuanza ujenzi wa mradi mkubwa wa maji ambao utasambaza huduma kwa wananchi zaidi ya 10,000 katika kata ya Kitere wilayani humo.
Hatua hiyo ni miongoni mwa mikakati ya wakala huo kusanifu na kujenga miradi mipya, ili kufikia lengo la kupeleka huduma ya maji kwa wananchi vijijini kwa asilimia 85 ifikapo 2025.
Meneja wa wakala huo Wilaya ya Mtwara, Mhandisi Hamisi Mashindike, amesema hayo leo wakati akizungumzia hali ya upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo.
Amesema ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha ujao na kwamba tayari wameshapata kibali na kutenga fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji.
Mashindike amesema kwa sasa hali ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Mtwara ni asilimia 57.6.
Amesema kuna miradi mingine inaendelea kujengwa yenye thamani ya Sh bilioni 5.06, ambayo itahudumia wananchi 32,717 baada ya kukamilika.