SERIKALI imetumia jumla ya Sh 293,050,508.58 kutoka Mfuko wa Mapambano dhidi ya Uviko-19 (TCRF), ili kumaliza kero ya maji kwa wananchi wapatao 10,448 wa vijiji vya Nzera na Bugando, Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Meneja wa Wakala wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Geita, Mhandisi Sande Batakanwa alibainisha hayo katika hafla ya uzinduzi wa mradi huo.
Mhandisi Batakanwa amefafanua kati ya fedha hizo, gharama ya mkandarasi ni Sh 258,676,096.58, gharama za mzabuni wa bomba Sh 23,181,003 na mzabuni wa pampu Sh 11,193,409.

Amesema mradi huo unajumuisha tenki la kuhifadhi lita 100,000 za maji na mtambo wa pampu wenye uwezo wa kusukuma lita 3,306 kwa saa, mtandao wa Km 6,679 na vituo 10 vya kuchotea maji.
Ameeleza, mradi huo ulianza kutekelezwa Desemba 2021 na kukamilika Desemba 2022 na mpaka sasa upo katika hatua ya matazamio na unatarajiwa kuboresha huduma maeneo hayo ya Geita vijijini
“Mradi huu unasimamiwa na Chombo cha Usimamizi wa Utoaji Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO). Chanzo cha maji katika mradi huu ni kisima cha maji chenye kina cha mita 50,” amesema.
Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Kasheku (msukuma) amewataka wananchi kuunga mkono mradi kwa kuunganisha maji nyumbani mwao na kuchangia kwa kulipa gharama kidogo ya maji.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amesema kwa kipindi cha miaka miwili (2022 na 2023) mkoa umepokea zaidi ya Sh bilioni 12 kuboresha huduma ya maji kati yake Sh bilioni mbili kwa ajili jimbo la Geita vijijini pekee.