Mradi wa maji kunufaisha vijiji 13 Newala
ZAIDI ya wakazi 20,000 kutoka katika vijiji 13 Wilaya ya Newala, mkoani Mtwara watanufaika na mradi wa uboreshaji wa huduma za maji pembezoni mwa mji wa Newala unaogharimu zaidi Sh Bilioni 2.
Akizungumza leo wakati mbio za Mwenge wa Uhuru ulipotembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Lidumbe, Dadi Samli, amesema mradi huo umekuja kumaliza kero ya maji iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa vijiji hivyo.
“Huduma ya maji kwa miaka mingi ilikuwa ni usumbufu na kero kubwa kwa watu wa maeneo haya, sasa ujio wa huu mradi ni ukombozi mkubwa kwetu, ” amesema.
Mwajuma Ally Mkazi wa kijiji hicho, amesema kwa kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini wanatumia maji hayo, hivyo wameondokana na changamoto hiyo kwa sasa.
“Kabla ya mvua hizi kunyesha tulikuwa tunapandisha mlima tunavuka kwenda huko chini kuchota maji ni hatua kidogo kutoka hapa hadi huko, kwa hiyo ujio wa mradi huu tunasema asante sana kwa serikali, utaturahisishia kupata maji kwa karibu na rahisi zaidi,” amesema.
Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini na Mijini (RUWASA), Wilaya ya Newala Mhandisi Nsajigwa Sadik, amesema mradi huo umefikia asilimia 85 na unatarajia kukamilika Aprili 30 mwaka huu.
Vijiji 13 vya kata za Mkunya, Mtumachi, Mcholi 1 na Mcholi 2 wilayani Newala ndiyo vitakavyofaidika na mradi huo.