Mradi wa maji kunufaisha wakazi 3,465 Mtwara

Mradi wa maji kunufaisha wakazi 3,465 Mtwara

WAKAZI  3,465 watanufaika na mradi wa ujenzi wa maji, ambapo kati ya hao 1,593 kutoka Kijiji cha Mwindi na 1872 Kijiji cha Mbawala Halmashauri ya  Wilaya ya Mtwara, ambao umegharimu zaidi ya Sh Milioni 800.

Akizungumza leo wakati Mwenge wa Uhuru ulipotembelea kwenye Halmashauri hiyo kwa ajili ya kukagua, kuweka mawe ya msingi miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo  huo wa maji, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwindi, Issa Namwewe amesema kabla ya mradi huo wakazi hao walikuwa wakitumia maji kupitia visima vya kienyeji, hivyo ujio wa mradi kwa sasa watakuwa wameondokana na changamoto hiyo.

Amesema siku za nyuma wakazi Kijijini hapo walikuwa wakiondoka usiku kwenda kutafuta maji porini, hali iliyosababisha baadhi yao kupata matatizo ya kukimbizwa na wadudu wakiwa wamebeba ndoo za maji kichwani, lakini leo hii wanajivunia maendeleo yanayoletwa na Serikali katika maeneo yao.

Advertisement

“Hapo zamani dada zetu, mama zetu walikuwa wanaondoka usiku kwenda porini huko  kusaka maji, basi walikuwa wanafukuzwa na wadudu, huku wakiwa na ndoo kichwani, leo hii nashukuru hajaenda mtu porini huko kusaka maji kwa sababu huduma ya maji tunapata kwa urahisi tofauti na siku za nyuma,” amesema.

Mwenyekiti huyo ameipongeza Serikali kwa jitihada hizo kubwa wanazozifanya kwa wananchi wa maeneo hayo na mengine kuhakikisha wanaboresha  na kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi, lakini pia kuwarahisishia kupata maji.

Akizungumza Zainabu Mpiku mkazi wa Kijiji cha Mwindi alisema: “Kuwepo kwa huu mradi kuna faida kubwa sana kwa sababu tulikuwa tunapata maji mbali, tulikuwa tunakutana na wanyama wakali ila sasa tunashukuru sana Serikali kutuletea huu mradi  mana tulikuwa tunachota maji ya visima huko porini.”

Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini na Mijini (RUWASA) Wilaya ya Mtwara,  Mhandisi Hamis Mashindika, amesema mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na umezingatia sera ya maji ya kumtua mama ndoo kichwani na mpaka sasa kaya 21 na taasisi 7 zimeunganishiwa huduma ya maji, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Hanafi Msabaha, amesema lengo la serikali ni kuhakikisha huduma hiyo ya maji inafikia angalau kwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Kitaifa Abdallah Shaib Kaimu, amesema Serikali imepeleka fedha nyingi katika mradi huo wa maji kwa ajili ya kuwasaidia wananchi hao, kwani maji ni  uhai na wanaendelea kuimarisha afya zao, hivyo amewaomba kuendelea kuutunza mradi huo, ili uendelee kuwasaidia kwa ajili ya vizazi vyao vya sasa na baadae, huku akiridhia hatua nzuri ulipofikia ujenzi huo na kuweka jiwe la msingi.