Mradi wa maji Makongo -Bagamoyo wafikia 87%

Huduma za maji safi

MRADI wa maji wa Makongo hadi Bagamoyo umefi kia asilimia 87 ili ukamilike ukiwa unagharimu Sh bilioni 65.4. Mkurugenzi wa Miradi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), Ramadhani Mtindasi alisema mradi huo utakamilika Desemba na kuhudumia wananchi zaidi ya milioni moja.

Kukamilika kwa mradi huo ni neema kwa wakazi wa Makongo, Goba, Tegeta, Mbweni hadi Mapinga wilayani Bagamoyo. Akizungumza katika ziara ya kamati ya siasa ya Mkoa wa Dar es Salaam, Mtindasi alisema mradi huo una matangi matatu ya maji yaliyopo Vikawe, Mbweni na Tegeta A.

Alisema mradi huo ambao umeanzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ukiwa na kilometa 1,250, unatekelezwa kupitia wafadhili wa maendeleo chini ya usimamizi wa Dawasa kupitia Mkandarasi wa Kampuni ya CDEIC & Hainan Joint Venture.

Advertisement

“Yanajengwa matangi matatu makubwa ya kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita milioni tano pamoja na ujenzi wa vituo viwili vya kusukuma maji vinavyojengwa eneo la Vikawe na Mbweni,” alisema.

Utakapokamilika, wateja 60,000 wa maeneo mbalimbali ya Changanyikeni, Vikawe, Goba, Mivumoni, Mbweni, Madale, Tegeta A, Bunju, Wazo, Ocean Bay, Salasala na Bagamoyo watanufaika.

Kwa upande wa Bagamoyo, utahudumia wakazi wa kata za Mataya, Sanzale, Migude, Ukuni, Mtambani, Nianjema, Kimara Ng’ombe na Vikawe Bondeni.

Alisema kwa upande wa Mabwepande, mradi utahudumia kata ya Mapinga, Salasala, Goba, Kinzudi, Mbezi na Kilongawima.

Kwa mujibu wa Mtindasi, lengo la Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni kufikia asilimia 95 ya usambazaji maji kwa upande wa mjini na asilimia 85 kwa upande wa vijijini. Dawasa wanatarajia kufikia asilimia 100 mwaka 2025. Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Adam Ngalawa alisema wameridhika na utekelezaji wa mradi.

Aliitaka Dawasa kuongeza kasi miradi ikamilike kwa wakati. Alimpongeza Rais Samia Suluhu kwa kutoa Sh bilioni 65 kukamilisha miradi ya maji ambayo ilianza wakati wa Awamu ya Tano.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe aliwataka wananchi kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake kuhakikisha miundombinu ya maji inalindwa. Mkazi wa Mabwepande, Saida Gerald Lusato aliishukuru serikali kuwafikishia huduma ya maji ambayo eneo hilo walikuwa na changamoto kubwa ya maji takribani miaka 10.​​​​​​​