Mradi wa Maji Ziwa Victoria wanukia

MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (MAUWASA) inategemea kuanza ujenzi wa mradi wa maji utakao unganisha eneo la Wilaya hiyo kupitia mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria.

Mradi huo utaanzia  eneo la Malampaka na kuelekea katika maeneo mengine ya Wilaya hiyo.

Akitoa Taarifa hiyo, leo Novemba 11, 2022 Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (MAUWASA), Mhandisi Nandi Mathias amesema  mradi huo utaweza kuwahudumia wakazi  80,000 wa wilaya hiyo.

Advertisement

Amesema mradi huo utasaidia changamoto ya upatikanaji wa maji hususani maeneo ya vijijini.

Aidha ameongeza kuwa mradi huo wa maji kutoka Ziwa Victoria utaunganishwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mkoani Shinyanga (Shuwasa) ili kufikia wakazi wote wa maeneo yanayo unganisha mikoa hiyo  miwili.

Amesema  pia wanaendelea  na miradi ya uchimbaji wa visima virefu kwa maeneo mengine ambayo bado hayajafikiwa na huduma za maji  kwa wilaya ya Maswa kutoka katika chanzo kikuu cha Bwawa la New Sola maarufu kama Zanzui lililoko katika wilaya hiyo.

Amesema tayari Mauwasa imekamilisha ujenzi wa matanki ya kuhifadhia maji yenye uwezo wa kupokea lita milioni 1.2.