Mradi wa umeme wa JNHPP wafikia 94.7%

PWANI: Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema kuwa, utekelezaji wa  mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha megawati 2,115 kwa sasa umefikia asilimia 94.78 huku mashine mbili za kuzalisha umeme zikiwa tayari zimeshafungwa kwa ajili ya kuanza kuzalisha umeme.

Dk Biteko amesema hayo  Desemba 28, 2023 wakati alipofanya ziara ya kukagua mradi huo wilayani Rufiji akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Mwenyekiti wa Kamati aliyoteua Rais ya ufuatiliaji mradi wa JNHPP, Profesa Idris Kikula, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO.

” Hatua iliyopigwa ya utekelezaji wa mradi huu kila mtu ameona kuwa ni kubwa kwenye hatua zote, mfano kwenye ujazaji maji wa bwawa la kuzalisha umeme, maji yamejaa kwa kiwango ambacho yanaruhusu kuzalisha umeme,

Pia ufungaji wa mashine ambazo zitatumika kuzalisha umeme, nafurahi kusema kuwa mashine mbili zimeshafungwa ambazo ni mashine namba tisa na namba nane na tunaamini kwamba mashine nyingine zitaendelea kufungwa kadri muda  unavyoenda ili kupata megawati zote 2,115.” Amesema Dk Biteko

Aidha,Dk. Biteko amesema kufungwa kwa mashine hizo mbili kunatoa matumaini ya kutekeleza agizo la Rais, Dk Samia Suluhu Hassan la kupunguza changamoto za umeme nchini ndani ya miezi sita ambapo sasa imebaki miezi mitatu ya utekelezaji wa agizo hilo kwani mashine hizo zitazalisha megawati 470 na kuingizwa katika gridi ya Taifa ili kuongeza kiwango cha umeme.

Katika hatua nyingine, Dk Biteko amesema kuwa, ni kweli kuna changamoto ya umeme hivyo kipaumbele kwa sasa ni kujikita katika kupata umeme wa uhakika na wananchi wana haki ya kujua hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ili kuondoa changamoto hiyo.

Aidha,Waziri Biteko amesema ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika mabwawa ya uzalishaji umeme,  ameelekeza TANESCO kuwa sehemu ya mkakati ya utunzaji mazingira, kwani baadhi ya watu wanachepusha mito na kuharibu mazingira hali ambayo inapelekea hadi umeme kutozalishwa wa kutosha na anayelaumiwa ni TANESCO hivyo amelitaka shirika hilo kutenga fedha za kutosha ila kila mdau anayehusika katika usimamizi wa mazingira ahusishwe.

Gharama za utekelezaji mradi wa JNHPP ni Trilioni 6.5 na Serikali imeshamlipa mkandarasi kampuni ya JV Elsewedy na Arab Contractors shilingi Trilioni 5.76 ambayo ni sawa na asilimia 87.83.

 

Habari Zifananazo

Back to top button