Mrema azikwa, amwagiwa sifa

SERIKALI imesema inathamini mchango wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema katika kukuza vyama vya upinzani nchini.

Aidha, serikali inatambua mchango wa marehemu Mrema ambaye katika serikali ya awamu ya pili alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na alianzisha mfumo unaosaidia changamoto za wanawake na sasa dawati la jinsia na watoto.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, George Simbachawene alisema hayo katika ibada ya mazishi ya marehemu Mrema ambaye alifariki dunia hivi karibuni jijini Dar es Salaam katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mrema amezikwa nyumbani kwake Kijiji cha Kiraracha, Marangu wilayani Moshi vijijini ambapo wanasiasa, wafanyabiashara, viongozi wa serikali na wananchi kwa ujumla walishiriki mazishi hayo.

Simbachawene alisema Mrema alikuwa muasisi wa mageuzi pale alipohama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuhamia chama cha NCCR-Mageuzi na kuwa miongoni mwa Watanzania waliohamasisha mfumo wa vyama vingi nchini.

Simbachawene alisema Mrema anakumbukwa kama waziri aliyeacha alama kwa kuanzisha vituo vidogo vya polisi nchini na vikundi vya ulinzi shirikishi maarufu wakati wake kama sungusungu.

Akizungumza kwa niaba ya vyama vya upinzani, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Feeman Mbowe alisema Mrema alikuwa na uthubutu wa mambo.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alisema yeye ni miongoni mwa wanasiasa waliolelewa na marehemu Mrema.

Alisema alikuwa Katibu wa Vijana wa CCM Moshi vijijini na wakati huo Mrema alikuwa mbunge wa Moshi vijijini na Waziri wa Mambo ya Ndani.

Akiongoza ibada ya mazishi, Padri Deogratius Masiika alisema Mrema alikuwa mpatanishi na mtetezi wa wanawake.

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button