Msaada wa kisheria kwa wanyonge waja

WIZARA ya Katiba na Sheria inaanzisha kampeni ya misaada ya kisheria iliyopewa jina la Rais Samia Suluhu Hassan kuthamini mchango wake katika kusimamia haki za wananchi.

Waziri wa Wizara hiyo, Dk Damas Ndumbaro amesema kampeni hiyo imeandaliwa na wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau wakiwamo kutoka sekta binafsi.

Kupitia akaunti yake katika mtandao wa kijamii wa twitter, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alieleeza kuwa Dk Ndumbaro ameeleza hayo alipozungumza kupitia Clubhouse ya Msemaji Mkuu wa Serikali.

“Tunakwenda kuhakikisha kwamba wanyonge na ambao hawawezi kumudu gharama za mawakili na wanasheria mbalimbali wanakwenda kuipata huduma hiyo,” alisema Dk Ndumbaro na kuongeza:

“Tunakutana chini ya mwamvuli mmoja unaoitwa ‘Mama Samia Legal Aid Campaign’.

“Na tuliamua kufanya hivyo kwa sababu juhudi hizi za msaada wa kisheria na kupigania haki za watu zimekuwa zikifanywa na wadau mbalimbali, serikali imefanya, wadau wa sekta binafsi wamefanya”.

Alisema pamoja na juhudi hizo, hakukuwa na juhudi za pamoja kuziratibu, hivyo serikali imeamua kuunganisha nguvu kuwezesha wananchi kupata haki.

Dk Ndumbaro alisema kumekuwa na malalamiko kuhusu ukiukwaji wa maadili na uvunjifu wa sheria ukiwamo ukatili wa kijinsia, haki za binadamu, migogoro ya ardhi, ndoa, mirathi na mengine.

“Watanzania wamekuwa wakilalamikia kuhusu kupata haki zao kwa hiyo sasa mkakati huu wa Mama Samia Legal Aid Campaign unakuja kugusa maeneo hayo ili kuwapatia Watanzania kile ambacho wanastahili katika sekta hiyo ya haki na sheria”alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button