Msako wanaonunua vifaa vya wizi Dar waja

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amesema kwa siku nne sasa tangu kuanza kwa operesheni ya kukabiliana na vijana wahalifu maarufu kama Panya Road, hali ni shwari mkoani humo, huku akisema kinachofuata sasa ni msako kwa wafanyabiashara wanaonunua vifaa vya wizi.

Amesema katika siku nne hizo, Polisi imefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 135, pamoja na vifaa mbalimbali vilivyoibiwa.

Makalla alisema hayo wakati wa kikao kazi Cha Kamati ya Ulinzi na Usalama kilichoketi kufanya tathmini ya hali ya usalama, pamoja na kupokea taarifa ya mwenendo wa operesheni ya kukamata wahalifu.

Ili kuhakikisha matukio hayo hayajirudii, alitaka vituo vya Polisi kufanya kazi kwa saa 24, ongezeko la doria, kila kata, kila mtaa kufanya mkutano maalum ya kujadili ajenda ya ulinzi kika wiki ya kwanza kila mwezi, ikiwa ni miongoni mwa mipango ya kudhibiti uhalifu.

Alisema mipango mingine ni msako kwa wafanyabiashara wanaouza na kununua vifaa vya wizi, kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi, ufuatiliaji wa mienendo ya wafungwa waliomaliza kutumikia vifungo na msako kwenye vijiwe, nyumba zisizokamilika (mapagala) na vibandaumiza, ambavyo vimekuwa sehemu ya kukutana na kuweka mipango.

Pamoja na hayo Makalla alitoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanazingatia suala la malezi kwa kufuatilia mienendo ya watoto wao.

Habari Zifananazo

Back to top button