MSD yaongeza upatikanaji dawa muhimu

BOHARI ya Dawa (MSD) imeeleza kuwa upatikanaji wa dawa muhimu nchini umeimarika kutoka asilimia 52 kipindi cha Januari mwaka jana hadi asilimia 72 Desemba mwaka huo.

Aidha, imesambaza vyandarua 3,442,972 vyenye thamani ya Sh bilioni 23.9 kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya mama na mtoto. Hayo yamo katika taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai katika kipindi cha miezi mitano kuanzia Oktoba mwaka jana hadi Februari mwaka huu ikielezea mambo ambayo yamefanywa na taasisi hiyo ya umma.

Kwa mujibu wa Tukai, pia kuna kuimarika kwa upatikanaji wa bidhaa muhimu za meno kutoka asilimia sifuri kipindi cha Januari 2022 hadi kufikia asilimia 100 kwa kipindi cha Desemba mwaka jana. Alisema pia walisambaza vyandarua kwa wanafunzi wa shule za msingi vyenye thamani ya Sh bilioni 6.2 kwenda mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa, Njombe, Dar es Salaam na Singida.

Advertisement

Aliyataja mambo mengine yaliyofanyika katika kipindi hicho kuwa ni kusambaza bidhaa za afya za miradi misonge zenye thamani ya Sh bilioni 224.2 kuanzia Julai hadi Desemba, 2022 ambazo hutolewa bure kwenye vituo vya kutolea huduma za afya. “Bidhaa hizi zinahusika na kupambana na kifua kikuu na ukoma, Ukimwi, malaria na magonjwa yasiyoambukizwa (NCDs),” alieleza Mkurugenzi Mkuu wa MSD.

Aliongeza kuwa pia wamesambaza vifaa za CEmONC katika vituo vya kutolea huduma 274 ambavyo vifaa 256 (asilimia 74) kati ya 345, vilisambazwa ili kuboresha uzazi salama na afya ya mama na mtoto. CEmONC ni vifaa vya kuwezesha uzazi pingamizi kwa wajawazito na watoto wachanga wanaozaliwa.

Aidha, Tukai alisema walitunza na kusambaza chanjo za thamani ya Sh bilioni 5.7 kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2022 za kuwakinga watoto na magonjwa mbalimbali yakiwamo polio na magonjwa mengineyo. Alizitaja miongoni mwa chanjo zilizosambazwa ni BCG (chanjo ya kumkinga mtoto na kifua kikuu), chanjo dhidi ya surua na chanjo ya kukinga kansa ya shingo ya kizazi.

Alibainisha kuwa pia walifunga mashine 2,315 za vifaa vya maabara na usambazaji wa vitendanishi vyake katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kuimarisha huduma ya vipimo vya uchunguzi. Tukai alieleza kuwa mashine hizi zitakuwa na faida kadhaa ikiwamo kusogeza huduma kwa wananchi; kupunguza gharama za uchunguzi na kuongeza upatikanaji wa huduma tajwa kwenye vituo ambavyo awali havikuwa na huduma hizo hivyo kuhakikisha wananchi wanafanyiwa uchunguzi kwa wakati.

Pia MSD imeendeleza sera ya viwanda kwa kujenga viwanda vya uzalishaji wa bidhaa za afya ili kupunguza utegemezi na uchelewaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi. “Kiwanda cha Barakoa kinafanya kazi na kiwanda cha mipira ya mikono (glovu) kinatarajia kukamilika mwezi Juni, 2023.

Kiwanda cha mipira ya mikono kinategemea kuzalisha mipira ya mikono milioni 86.4 kwa mwaka na mahitaji ya nchi ni milioni 104 kwa mwaka,” alieleza. Alibainisha kuwa kiwanda hicho kitazalisha asilimia 83.4 ya mahitaji hayo.

“Matarajio ni kwamba mipira ya mikono itawakinga watoa huduma za afya na maambukizi mbalimbali hivyo kuwafanya watoe huduma kwa usalama. Kiwanda cha mipira ya mikono kinatarajia kuwanufaisha wananchi wa Njombe kwa kutengeneza ajira zaidi ya 200 zile za moja kwa moja na zile zisizo za moja kwa moja,” alieleza. Kiwanda hicho cha mipira ya mikono kipo Idofi mjini Makambako mkoani Njombe.

Aidha, wameandaa andiko la uanzishaji wa kampuni tanzu itakayosimamia uendeshaji wa viwanda kwa ufanisi. “Mfumo huu utasaidia kampuni kukua, kuweza kuzalisha bidhaa za aina tofauti, kuingia ubia na makampuni mengine na kuwezesha uzalishaji wa ndani ya nchi hivyo kuepusha nchi na ukosefu wa bidhaa za afya pale ambapo majanga yanajitokeza,” alibainisha bosi wa MSD.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *