Mshindi wa Maisha Plus 2016 awa mwalimu wa Gym nchini Kuwait

MSHINDI wa Shindano la Maisha Plus 2016 raia wa Kenya, Olive Kiarie amewataka mashabiki zake waliokuwa wakimfuatilia kupitia shindano hilo wamsapoti katika kazi yake mpya ya ualimu wa mazoezi na kunyanyua vitu vizito.
Olive kwa sasa anaishi na kufanya kazi nchini Kuwait katika moja ya Gym kubwa nchini humo akiwa kama mwalimu msaidizi wa mazoezi katika kituo hicho cha mazoezi (gym).
“Kwa sasa nafanya kazi nchini Kuwait na nimekuwa mwalimu wa mazoezi katika moja ya Gym kubwa nchini hapa, na nafanikiwa kwa kuwa nafanya kitu nachokipenda,” amesema Olive.
Olive amesema kabla hajashinda Sh milioni 30 za Kitanzania mwaka huo wa 2016 katika mashindano hayo alikuwa akipenda michezo ndiyo maana aliporudi kwao alijiendeleza katika michezo hasa ya kutengeneza mwili na kunyanyua vitu vizito.
“Napenda sana michezo baada ya kurudi Kenya nwaka uliofuata nilijikita katika michezo nikaanza kidogo kidogo kunyanyua vitu vizito na kutengeneza mwili wangu nikaenda kusomea ualimu wa michezo hadi nikapata kazi nchini Kuwait na sasa nina muonekano huu,” amesema Olivie.
Olivie amesema baada ya kufanya mazoezi kwa muda mrefu mwaka 2020 aliamua kwenda shule ya ualimu wa mazoezi na mwaka 2021 akawa mwalimu hadi akapata kazi nje ya nchi yao na sasa yeye ni mwalimu wa mazoezi na maisha yake kwa muda mrefu ni mazoezi.
“Mashabiki zangu waliokuwa wakinifuatilia kwenye Maisha Plus kwa sasa naomba wanisapoti kupitia kazi yangu mpya ya ualimu wa mazoezi kupitia page zangu nao watajifunza kitu” ameeleza Olive.