‘Mshitakiwa alitambuliwa katika gwaride la utambuzi’
MKAGUZI Msaidizi wa Jeshi la Polisi katika Kituo cha Kijitonyama, Jesca Malia (37), ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi mlalamikaji alivyomtambua mshitakiwa aliyemuwekea kilevi, kisha kumuibia mali zake.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Mosie Kaima katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu juzi, Malia alidai mlalamikaji ambaye ni Consolatha Alphonce, alimtambua mshitakiwa katika gwaride la utambuzi.
Malia alitoa ushahidi dhidi ya Borgias Augustine na wenzake wawili mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Ramadhani Rugemarila anayesikiliza kesi hiyo.
Alidai Februari 21, 2022 mchana, alikuwa Kituo cha Polisi Kijitonyama akiendelea na majukumu yake ya kazi, alipigiwa simu na mpelelezi Mayunga kuwa kuna mlalamikaji ambaye kesi yake ipo kwake kuwa anaweza kumtambua mshitakiwa kwa sura.
Alidai kuwa alimueleza mlalamikaji ambaye ni Consolatha aende kesho yake kituoni hapo kwa ajili ya gwaride la utambuzi.
Malia alidai Februari 22, 2022 mchana, Mayunga alifika kituoni hapo akiwa na Alphonce na alimwelekeza ampeleke kwenye chumba maalumu ili na yeye atafute askari wa kusimamia gwaride.
Alidai aliandaa gwaride la watu wanane ambao wanaendana na Augustine na kuwapanga mstari mmoja na mtuhumiwa akachagua kusimama mtu wa kwanza kutoka kulia.
Shahidi huyo alidai alijaza fomu ya utambuzi kwa kuandika majina ya watu wote waliokuwa kwenye gwaride likiwamo na jina la mlalamikaji Consolatha Alphonce, alipomaliza alimuita askari Ernest ili ampeleke shahidi.
“Shahidi aliweza kumtambua mtuhumiwa ambaye alimshika kwenye bega lake, ambapo nikamuita askari Ng’ande ili amtoe nje shahidi, baada ya hapo nikamalizia kujaza fomu sehemu ya utambuzi,” alidai shahidi.
Alidai baada ya utambuzi huo, mshitakiwa alirudishwa mahabusu na kuanza kuandaa maelezo kuelezea alichokisimamia.
Hakimu Rugemarila aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 10, mwaka 2023 kwa ajili ya kusikilizwa.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Agosti 23, 2021 mshitakiwa akiwa eneo la Hoteli ya Elegance iliyopo Sinza, ndani ya Wilaya ya Kinondoni kwa nia ovu alimwekea kilevi Consolatha.
Katika mashitaka ya pili, siku hiyo hiyo na eneo hilo mshitakiwa Augustine anatuhumiwa kuiba simujanja aina ya IPhone yenye thamani ya Sh milioni 2.9, nokia yenye thamani ya Sh 50,000 na kwa kupitia ATM kadi ya CRDB aliiba Sh 700,000 mali ya Consolatha.
Pia, katika mashitaka ya tatu yanawakabili Ally Kibuga na Abdallah Manti ambao wanatuhumiwa kupokea simu aina ya IPhone ambayo ilikuwa inajulikana kama imeibwa.