Mshtuko kifo cha Membe

Mshtuko kifo cha Membe

KUTOKANA na kifo cha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Rais Samia Suluhu Hassan amesema Membe alikuwa mtumishi wa umma mahiri.

Alisema hayo kupitia salamu zake za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kupitia ukurasa wake wa Twitter jana.

Rais Samia alisema kuwa kwa zaidi ya miaka 40, Membe alikuwa mtumishi mahiri wa umma, mwanadiplomasia, mbunge na waziri aliyeitumikia nchi yake kwa weledi.

Advertisement

“Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha ndugu Bernard Membe. Pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki. Mungu amweke mahali pema. Amina,” alisema Rais Samia.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alisema Membe alikuwa kiongozi mwenye uwezo mkubwa, mwanadiplomasia na mtumishi shupavu wa Taifa.

“Kwa masikitiko makubwa nimehuzunishwa na taarifa ya kifo cha Bernard Membe, natoa pole kwa familia, marafiki na wote walioguswa na msiba huu. Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani. Amina,” alisema Dk Mwinyi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara, Magdalena Sakaya alisema Membe alikuwa kiongozi mkaribishaji kwa kila mtu aliyemwendea kwa shida yoyote.

Sakaya alisema alimfahamu Membe tangu wakiwa bungeni mwaka 2005 hadi 2015 na wakati wote alipokuwa Waziri alikuwa msikivu kwa wabunge wenzake waliomweleza shida zao, alikuwa mcheshi, mwenye upendo na mwenye ushirikiano.

“Kama Taifa tumepoteza kiongozi, mwanasiasa na Mtanzania aliyeacha alama kwa Taifa, aliwajibika vyema katika nafasi yake kama kiongozi,” alisema Sakaya.

Mwenyekiti mstaafu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (CCM), Dk Edmund Mndolwa alisema kifo cha Membe ni msiba mzito kwa nchi.

Dk Mndolwa alisema Membe alikuwa kiongozi shupavu, aliyejiamini na hakuwa muoga, hivyo kifo chake ni msiba mzito kwa Taifa.

“Ni msiba mzito wa nchi, unasikitisha ni wa ghafla, Mungu hana makosa, ni Muumba wetu, anachukua kiumbe chake anapokitaka, kwa hiyo hatumlaumu Mungu, lakini tunasikitika, tunamwombea mwenzetu awekwe mahali pema peponi na tunaiombea familia yake wawe na subira, kwa kweli ni msiba mzito,” alisema Dk Mndolwa.

Naye Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe katika salamu zake za rambirambi kupitia ukurasa wake wa Twitter, alisema Membe alikuwa mwanasiasa mahiri, mwanadiplomasia maarufu na mwakilishi wa wananchi.

Alisema hakuna maneno yanayoweza kueleza mshtuko alioupata kutokana na taarifa za msiba huo, hivyo alimshukuru Mungu kwa maisha ya Membe.

“Kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Wanachama wa Chama cha ACT-Wazalendo ambaye Bernard Membe aliwahi kuwa mwanachama wake, natoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wote wa Jimbo la Mtama,” alisema Zitto.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe alisema amepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Membe na kuongeza kuwa: “Membe alitumikia nchi yetu katika ngazi mbalimbali na alikuwa hazina muhimu kwa taifa.”

Katika hatua nyingine Daktari wa familia ya Membe, Harun Nyagori akizungumzia kifo cha Membe kilichotokea jana katika Hospitali ya Kairuki mkoani Dar es Salaam, alisema Membe amefariki kifo cha kawaida na kuwataka watu wapuuze taarifa zinazoenea mitandaoni kuwa ameuawa.

D Harun alisema: “Membe miaka yote amekuwa na afya hakuwahi kuwa na ugonjwa wowote au magonjwa sugu kama kisukari, magonjwa ya moyo, presha hakuwahi kuwa nayo… juzi alipata homa ndogo ya kifua, akipata shida ya kukohoa na kubanwa kifua na ilipofika usiku wa kuamkia alfajiri ya jana alishindwa kupumua ghafla akakimbizwa hospitali.

“Kwa kifupi maradhi haya yanatokana na virusi ambavyo vinazunguka vinaingia kwa njia ya hewa, vinasababisha mgando kwenye mfumo wa mapafu, damu inakuwa nzito hiyo ndio sababu ya kifo chake. Tuondoe mawazo potofu ambayo yamekuwa yakizungumzwa mtandaoni kwamba aidha ameuawa au amepewa sumu na vitu kama hivyo, amekufa kifo cha kawaida ambacho mtu yeyote aidha mimi au wewe kinaweza kumpata.”

Kuzaliwa

Kwa mujibu wa Blogu ya Chama Cha Mapinduzi, Membe alizaliwa Novemba 9, 1953 katika Kijiji cha Rondo-Chiponda mkoani Lindi akiwa mtoto wa pili kati ya watoto saba katika familia ya Kamillius Ntachile na Cecilia Membe.

Elimu

1962–1968: Elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chiponda mkoani Lindi.

1969–1972: Elimu ya sekondari katika Shule ya Seminari Namupa, Lindi.

1973–1974: Kidato cha tano na sita katika Shule ya Seminari Itaga, Tabora.

1975–1980: Aliajiriwa serikalini, Ofisi ya Rais.

1981–1984: Alipata Shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

1985–1989: Aliendelea na ajira yake serikalini katika Ofisi ya Rais.

1990–1992: Alipata Stashahada ya Uchumi, Uhusiano wa Kimataifa na Sheria za Kimataifa katika Chuo Kikuu cha John Hopkins.

1993–1994: Alirudi serikalini kuendelea na kazi kama mchambuzi wa masuala ya ulinzi na usalama.

Mafunzo

Kati ya mwaka 1975 na 1976 alijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kambi ya Oljoro, Arusha.

Mwaka 1978 alipata mafunzo ya sheria za jinai na usalama wa nchi, nchini Uingereza.

Mwaka 1980 alipata mafunzo ya siasa katika Chuo cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kivukoni, Dar es Salaam ambacho sasa ni Chuo cha Mwalimu Nyerere.

Familia

Mwaka 1986 alifunga ndoa na Dorcas Masanche katika Parokia ya Mtakatifu Joseph Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam na kujaliwa kupata watoto watatu, Cecilia, Richard na Denis.

Siasa

Kuhusu siasa, Membe alishika nafasi mbalimbali ikiwemo Kamanda wa Vijana wa Mkoa wa Lindi, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa na Katibu wa Sekretarieti ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Mtama kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) nafasi ambayo alichaguliwa tena mwaka 2005 na mwaka 2010 hadi alipostaafu ubunge mwaka 2015.

Januari 2006, aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani na katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri mwezi Oktoba mwaka 2006, alihamishwa Wizara na kuwa Naibu Waziri Nishati na Madini.

Januari 2007, Rais Kikwete alimteua Membe kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa baada ya aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo, Dk Asha-Rose Migiro kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Membe alihudumu katika nafasi hiyo kuanzia mwaka 2007 hadi 2015.

Kutambuliwa

Kwa kutambua mchango wake katika kurejesha amani na utulivu katika Visiwa vya Comoro mwaka 2008, Membe alikuwa miongoni mwa Watanzania waliotunukiwa Nishani ya Operesheni Demokrasia Comoro na Rais Kikwete.

Uzoefu

2006–2015: Alikuwa Mjumbe wa Baraza la Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

2008–Mwenyekiti Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Afrika, Addis Ababa, Ethiopia. Pia alikuwa Mkuu wa waangalizi wa uchaguzi mkuu wa Zimbabwe kutoka Jumuiya ya SADC.

2006–2011: Katibu wa Sekretarieti ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, CCM.

2006–2011: Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa.

2006–2017: Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, Taifa.

2013–2015: Mwenyekiti Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Madola ‘Commonwealth’.

2014–2015:Mwenyekiti Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *